Dondoo

Jombi asema ‘naacha kazi nisipopewa asali’

March 7th, 2018 1 min read

Na BENSON MATHEKA

NYAYO ESTATE, EMBAKASI

BUDA mmoja mtaani hapa aliwashangaza rafiki zake kwa kutishia kuacha kazi akidai mkewe alikuwa akimnyima uroda.

Jamaa alikuwa kilabuni akiburudika na marafiki alipozama kwenye mawazo na wakamuuliza kilichokuwa kikimsumbua.

“Ninataka kuacha kazi kwa sababu sina amani katika boma langu. Mke wangu amekuwa akinikausha sana kwa shughuli. Kwa miezi mitatu sasa ameniruhusu kuonja tunda mara moja. Nataka niende kuishi ushago mbali sana na yeye,” jamaa alisema.

Baada ya marafiki kumdadisi, aliwaeleza kwamba mkewe huwa anarauka saa tisa usiku kila siku na kumuacha kwenye baridi kitandani akidai anaenda kazi. “

Mimi hushindwa ni kazi gani huwa anaenda alfajiri kwa sababu ofisi za kampuni yao hufunguliwa saa mbili asubuhi. Najua anampenda Mungu na anadai huwa anapitia kanisani lakini hata mimi nina haki kama mume.

Tabia yake imenifika shingoni na nimeamua kumuacha hapa mjini aendelee na shughuli zake nikiwa mbali,” jamaa alisema huku akibugia pombe kwa fujo.

Inasemekana baada ya kumsikiliza, marafiki waling’amua kwamba ndoa ya mwenzao ilikuwa na matatizo na alikuwa akipitia wakati mgumu sana.

Walimuacha akatulia kisha wakaahidi kumsaidia ili asiache kazi. “Walikubaliana kumtuma mke wa mmoja wao ambaye ni mshauri nasaha kumshauri mke wa jamaa amshughulikie mumewe kwa mahaba ili kumwepushia mateso ya akili na kimwili,” alisema mdokezi.

Inasemekana haikuwa mara ya kwanza jamaa huyo kukosana na mkewe japo hakuwa akiwaeleza marafiki zake.

“Mara kwa mara jamaa na mkewe wamekuwa wakigombana na hakuna aliyekuwa akifahamu chanzo cha mzozo wao hadi jamaa alipofungulia marafiki moyo wake,” alisema mdokezi.