Nabulindo aahidi kuunganisha wakazi wa Matungu

Nabulindo aahidi kuunganisha wakazi wa Matungu

Na SAMMY WAWERU

MBALI na kufanya maendeleo Matungu nitajikakamua kuunganisha wakazi kufuatia migawanyiko ya kisiasa iliyojiri, amesema mbunge mteule wa eneobunge hilo, Bw Peter Oscar Nabulindo.

Bw Nabulindo alisema hayo baada ya kutangazwa rasmi Ijumaa kama mshindi wa kiti cha ubunge Matungu, Kaunti ya Kakamega, kufuatia uchaguzi mdogo ulioandaliwa mnamo Alhamisi.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) ilitangaza kwamba Nabulindo na ambaye aliwania kiti hicho kwa tiketi ya chama cha ANC, kinachoongozwa na Bw Musalia Mudavadi, alizoa jumla ya kura 14, 257.

Kwenye kinyang’anyiro hicho kilichoshuhudia ghasia na vurugu, Nabulindo alifuatwa na Bw David Were (ODM) aliyepata kura 10, 565.

Chama cha UDA na kinachohusishwa na Naibu wa Rais, Dkt William Ruto, kiliwakilishwa na Bw Alex Lanya aliyepata kura 5, 513.

Uchaguzi huo mdogo ulivutia jumla ya wagombea 15.

“Lengo langu ni kuleta watu wa Matungu pamoja. Migawanyiko ya kisiasa, kijamii na kikabila isiwepo. Tuwe kama jamii moja,” akasema Bw Nabulindo, akishukuru kwa dhati wakazi waliomchagua.

Mbunge huyo mpya alisema katika siku za hivi karibuni migawanyiko ya jamii eneo la Magharibi mwa Kenya imeonekana kukita mizizi.

Aidha, Bw Nabulindo alihoji utengano huo unaendelea kuchochewa na wanasiasa.

“Kwa tulioshindana nao, wajiunge nasi ili tuweze kufanya maendeleo na kuimarisha maisha ya watu wa Matungu. Siasa zimeisha, ni wakati wa kazi,” akasema.

Nabulindo alisema ataipa kipau mbele miradi ya maendeleo iliyoanzishwa na mtangulizi wake.

Kiti cha Matungu kilisalia wazi baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa eneo hilo, Bw Justus Murunga, Novemba 2020.

You can share this post!

Bandari iko tayari kulima Nzoia Sugar

Tunakamatwa kwa sababu mtoto mwenye maono amezaliwa jijini...