Nabulindo aapishwa rasmi mbunge wa Matungu

Nabulindo aapishwa rasmi mbunge wa Matungu

Na CHARLES WASONGA

MBUNGE mpya wa Matungu Peter Oscar Nabulindo aliapishwa Alhamisi ili aweze kutekeleza majukumu yake rasmi kama mbunge.

Alilishwa kiapo katika hafla fupi iliyoongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi ndani wa ukumbi wa mijadala bungeni wakati wa kikao cha alasiri.

Bw Muturi alimpongeza mbunge huyo mpya kufuatia kuchaguliwa kwake katika uchaguzi mdogo uliofanyika Machi 4, 2021, na kukumbwa na visa kadhaa vya ghasia.

“Pongezi zaidi kwa kuchaguliwa na wakazi wa Matungu kuja kuwawakilisha kama Mbunge wao katika asasi hii ya bunge. Uwe huru kutekeleza majukumu kwa mujibu wa Katiba na sheria zinazoongoza shughuli za Bunge la Kitaifa,” akasema Bw Muturi.

Bw Nabulindo aliyedhaminiwa na chama cha Amani National Congress (ANC) alitangazwa mshindi kwa kuzoa kura 14,257 huku mpinzani wake wa karibu David Aoko Were wa ODM akiibuka wa pili kwa kura 10,555. Naye Alex Lanya wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) alishika nambari tatu kwa kupata kura 5,513.

Kiti hicho kilisalia wazi kufuatia kifo cha Bw Justus Murunga ambaye amekuwa mwakilishi wa eneobunge hilo tangu Novemba 17, 2017.

Kampeni za kuelekea uchaguzi huo zilishuhudia ushindani mkali kati ya wanasiasa ambao wanapania kumrithi Rais Uhuru Kenyatta kama Rais wa Tano wa Kenya.

Wanasiasa hao ni kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, kiongozi wa ODM Raila Odinga na Naibu Rais William Ruto waliotumia shughuli hizo kupima nguvu uwezo wao kuwavutia wapigakura wa eneo pana la Magharibi mwa Kenya.

You can share this post!

PSG wafuatilia hali ya Ronaldo kambini mwa Juventus kwa nia...

Zack Kinuthia afichua kuhusu mpango wa Sh5.6 bilioni kukuza...