Lugha, Fasihi na Elimu

Nafasi iliyopo ya ujasiriamali wa Kiswahili katika mtaala wa Umilisi

May 8th, 2024 1 min read

NA PROF JOHN KOBIA

MOJAWAPO ya masuala mtambuko yanayosisitizwa katika Mtaala wa Umilisi (CBC) ni ujasiriamali.

Ujasiriamali ni uwekezaji mtaji katika biashara. Mtaala wa umilisi hasa kuanzia Gredi ya 10 hadi 12 unatarajiwa kumwaandaa mwanafunzi kujiunga na chuo kikuu, chuo cha kiufundi, chuo cha kadri au ulimwengu wa ajira.

Inatarajiwa kuwa mwanafunzi ataweza kujiajiri. Hii ni kwa sababu inatarajiwa kwamba mafunzo atakayopata yanaweza kumwezesha kupata ujuzi wa kujipatia ajira au kujiajiri.

Kwa hivyo, ujasiriamali ni mojawapo ya masuala mtambuko yanayohimizwa katika mtaala wa CBC. Je, Kiswahili kina nafasi gani katika kufanikisha ujasiriamali?

Kiswahili kina nafasi muhimu katika ujasiriamali. Hii ni kwa sababu Kiswahili kimepewa majukumu muhimu na Katiba ya Kenya ya 2010, Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Mataifa.

Ujasiriamali unahusu mtu kutumia maarifa ili kupata mapato.

Ujasiriamali pia unahusu uwezo wa binadamu kubadilisha mawazo au fikra na kuwa vitendo vinavyoweza kumpa mtaji.

Kwa mfano, mtu anapotumia lugha ya Kiswahili kiusanii kuwachekesha watu na wanamlipa pesa huo ni ujasiriamali.

Mtu anapowaza kwa kina, kutunga novela ya Kiswahili na kuuzia wasomaji ni ujasiriamali.

Ujasiriamali huhitaji mtu mwenye ubunifu na ambaye yuko tayari kuwaza kwa kina ili kutatua matatizo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii katika jamii.

Lugha ya Kiswahili ina nafasi katika ujasiriamali katika mtaala wa umilisi.

Nafasi hii inaweza kutokea kupitia utungaji wa kisanii, tafsiri, ukalimani, uhariri, uandishi wa vitabu, mazungumzo ya papo kwa hapo, uhakiki na uandishi wa hotuba.

Haya yanapaswa kufunzwa katika Gredi ya 10 hadi 12. Kiswahili ni bidhaa na huduma inayoweza kutumiwa katika ujasiriamali ili kuendeleza jamii.