Habari Mseto

Nafasi ya Sakaja yajazwa

July 29th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

SENETA Maalum Sylvia Kasanga amechaguliwa awe mwenyekiti wa Kamati ya Seneti kuhusu Covid-19 kufuatia kujiuzulu kwa Seneta wa Nairobi Johnson Sakaja.

Bw Sakaja alijiondoa wiki jana kwa hiari kutokana na kisa cha aibu ambapo alikamatwa akibugia pombe katika kilabu cha Ladies Lounge baada ya saa za kafyu.

Alifikishwa katika mahakama na kutozwa faini ya Sh15,000 baada ya kukiri kosa hilo na kuomba msamaha hadharani.

Bi Kasanga ambaye aliteuliwa na chama cha Wiper katika Seneti alichaguliwa bila kupingwa katika uchaguzi uliofanyika Jumatano katika majengo ya bunge.

Bi Kasanga, ambaye alihudumu kama Naibu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, aliwapongeza wanachama wa kamati hiyo kwa kuonyesha imani katika uongozi wake.

“Kwa unyenyekevu mkubwa nawapongeza wanachama wa Kamati Maalum ya Seneti kuhusu Covid-19 kwa kuamua niwe mwenyekiti wao. Nitatekeleza majukumu ya wadhifa huu kuhakikisha kuna uwajibikaji katika vita dhidi ya janga hili miongoni mwa asasi zote za ngazi zote za serikali,” akasema.

Mnamo Jumanne, Seneta wa Bomet Christopher Lang’at aliteuliwa kuwa mwanachama wa kamati hiyo kuchukua nafasi ya Bw Sakaja.

Hoja ya kupendekeza jina lake iliwasilishwa na kiranja wa wengi Irungu Kang’ata na kuungwa mkono na maseneta wote.