Habari za Kitaifa

Nafuu kwa Raila washindani wake AUC wakipungua


WASHINDANI wa Raila Odinga katika uwaniaji wa Uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) wamepungua baada ya wawili waliomezea mate wadhifa huo kujiondoa huku orodha ya masuala ambayo kila mgombeaji amewasilisha ikionyesha changamoto za kudumu za muungano wa bara.

Kabla ya tarehe ya mwisho ya kuwasilisha wagombeaji ambayo ni Agosti 6, imeibuka kuwa Fawzia Adam wa Somalia na mgombea wa Ushelisheli Vincent Meritoni wameng’atuka kwenye kinyang’anyiro hicho, na kumuacha Raila Odinga wa Kenya kumenyana na Mahmoud Ali Youssouf wa Djibouti.

Maafisa wawili wa Serikali ya Somalia walisema kuwa Somalia haitamteua Bi Adam, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje kuwania kiti AUC, lakini wote wawili hawakutoa sababu.

Duru nyingine zilidai kuwa Somalia ilichagua kuunga mkono mgombea mwingine kutoka nchi tofauti.

Bi Adam mwenyewe hakujibu maswali ya Taifa Leo kuhusu ugombeaji wake.

Mnamo Julai 22, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ushelisheli ilithibitisha kuwa Bw Meriton, Makamu wa Rais wa zamani, alijiondoa katika kinyang’anyiro hicho, akitaja sababu za kiafya kuwa kiini cha hatua hiyo.

“Serikali ya Jamhuri ya Ushelisheli inapenda kuwafahamisha kwamba Bw Vincent Meriton, Makamu wa Rais wa zamani wa Jamhuri ya Ushelisheli, ameamua kutoendelea na azma ya kuwania Uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) katika uchaguzi utakaofanyika wakati wa Mkutano wa 38 wa Kawaida wa Muungano wa Afrika mnamo Februari 2025, kutokana na sababu za kiafya,” ilisema taarifa hiyo.

Huku muda wa kuwasilisha majina ya wagombeaji ukiwa Jumanne ijayo, inaonekana kinyang’anyiro hicho hadi sasa kitakuwa kati ya Bw Odinga na Bw Youssouf. Wote wawili waliwasilisha maombi yao kwa Wakili wa Kisheria wa Muungano wa Afrika mnamo Jumatatu, Julai 29.

Hata hivyo, kulikuwa na habari kwamba aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Nje wa Tanzania, January Makamba, anaweza kujiunga na kinyang’anyiro hicho. Bw Makamba na maafisa wa Serikali ya Tanzania hawakuthibitisha.

Chini ya kanuni za utaratibu, ilibidi wawaniani kwanza kuwasilisha stakabadhi kwa Mkuu wa Kanda ya Mashariki, ambaye ni Mwakilishi Mkuu wa Mauritius katika Muungano  wa Afrika, Dharmraj Busgeeth, na baadaye kwa Wakili wa Kisheria wa Tume ya AU. Kanda ya Mashariki itagombea kiti cha Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika, chini ya sheria mpya.

Mnamo Jumatatu, Wizara ya Masuala ya Nje na Masuala ya Wakenya Wanaoishi Ng’ambo ilisema imemteua Bw Odinga kwa sababu ana uzoefu wa kutosha kushughulikia changamoto za bara hili.

“Afrika inaendelea kukumbwa na dhiki ya kiuchumi, changamoto za kimazingira, migogoro, ugaidi na mizozo ya jumla ya kijamii, inayochochewa na ushindani wa kijiografia.

“Labda hakuna wakati wowote katika historia ya Muungano wa Afrika ambapo bara linahitaji kiongozi mwenye maono zaidi, mwanasiasa aliyekamilika na mtetezi wa Afrika,” Kenya ilisema.

Bw Odinga na mpinzani wake wa Djibouti wanalenga kutatua matatizo ya bara, ikiwa ni pamoja na yale ya AUC.

Bw Odinga anasema anataka kuangazia utangamano wa Afrika na maendeleo ya miundombinu, akitumia uzoefu wake kama Waziri wa zamani wa Kawi na baadaye Mjumbe Mkuu wa Muungano wa Afrika kuhusu Maendeleo ya Miundombinu.

Bw Youssouf aliahidi kutekeleza mambo kama hayo lakini pia alisema kuwa atatumia ushiriki wa sekta ya kibinafsi ili kutimiza matumizi ya Eneo Huru la Biashara ya Bara la Afrika (AfCTA), mkataba wa 2018 unaokusudiwa kupanua biashara ya ndani ya Afrika lakini ambao unahitaji kujengwa upya kwa miundombinu.