Habari Mseto

Nafuu tele marufuku ya mikoko ikiondolewa

February 20th, 2019 2 min read

Na KALUME KAZUNGU

SERIKALI ya kitaifa hatimaye imeondoa marufuku ya ukataji mikoko ambayo imedumu katika Kaunti ya Lamu kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Hatua hiyo ni afueni kwa zaidi ya familia 30, 000 ambazo hutegemea uvunaji wa mikoko ili kukimu mhitaji yao.

Akizungumza mjini Lamu wakati alipoongoza maafisa wengine wakuu wa Wizara ya Misitu katika ziara yao eneo hilo Jumanne, Naibu Afisa wa Masuala ya Uhifadhi wa Misitu wa Shirika la Misitu (KFS) nchini, Bi Charity Munyasia, alisema serikali imeafikia kuondoa marufuku hiyo katika Kaunti ya Lamu ili kuwawezesha wakazi kuendeleza uchumi wao.

Bi Munyasia, aidha aliwataka wakazi wa Lamu kuhakikisha wanatekeleza uvunaji mikoko katika hali endelevu ili misitu hiyo idumu Lamu.

Aliwashauri wakazi pia kupanda mikoko zaidi kila mara wanapoendeleza uvunaji wa miti hiyo ili isipungue.

Alisema KFS itashirikiana na idara ya usalama ili kuhakikisha sheria zote zinazoambatana na uhifadhi wa misitu zinafuatwa ipasavyo wakati mikoko itakapokuwa ikiendelea kuvunwa.

Bi Munyasia kadhalika aliweka wazi kwamba ni Kaunti ya Lamu pekee ambapo marufuku ya ukataji mikoko imeondolewa hali marufuku hiyo inaendelezwa kwenye maeneo mengine ya nchi.

“Tuko haoa Lamu leo kutangaza kuondolewa kwa marufuku ya mikoko. Tumeafikia hatua hiyo hasa baada ya kupokea vilio vya wakazi wa hapa ambao marufuku iliwaathiri pakubwa.

Nyumba za hapa Lamu, ambao ni mji wa kale pia zinaanguka kwa kukosa ukarabati.

Watoto pia wamekuwa wakikosa kwenda shule kwa ukosefu wa karo hasa baada ya kitega uchumi cha wakazi ambacho ni mikoko kufungiwa.

Tumefungulia mikoko na cha msingi ni wakazi kuwa makini wanapovuna miti hiyo.

Wahakikishe wanapanda mikoko kwa wingi wakati wanapotekeleza shughuli zao,” akasema Bi Munyasia.

Tangazo hilo limepokelewa kwa furaha na wakazi wa Lamu waliosema limekuja kwa wakati ufaao.

Mwenyekiti wa Muungano wa Wakataji Mikoko, Kaunti ya Lamu, Abdulrahman Aboud aliishukuru serikali kwa kuondoa marufuku ya mikoko.

“Tunafurahia kwamba marufuku imeondolewa. Ombi letu ni kwamba serikali inaposema imeondoa marufuku ni iwe imeondoa marukufu kweli.

Mara nyingi wamekuwa wakituambia marufuku imeondolewa na kisha tunakatazwa kuendeleza shughuli zetu,” akasema Bw Aboud.

Naye Bw Abdalla Hyder, alisema angalau ndoa zao zitadumu baada ya marufuku kuondolewa.

Kumekuwa na ripoti za talaka kuongezea katika Kaunti ya Lamu hasa tangu serikali ilipopiga marufuku biashara ya mikoko mnamo Februari mwaka jana.

“Wake zetu angalau watarudi nyumbani. Wengi walitoroka waume zao hasa baada ya kugundua kuwa kitega uchumi chao kimefungwa,” akasema Bw Hyder.

Aidha, kulishuhudiwa shamrashamra miongoni mwa wakazi wa maeneo ambako uvunaji mikoko huendelezwa kwa wingi, ikiwemo kisiwa cha Lamu, Manda, Kizingitini, Faza, Mkokoni na sehemu nyingine hasa punde taarifa za kuondolewa kwa marufuku ya mikoko zilipofikia vijiji hivyo.