Michezo

Nahodha wa Harambee Starlets atua kambini mwa Thika Queens kwa mkataba wa miaka mitatu

December 3rd, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha Thika Queens kinachoshiriki Ligi Kuu ya Soka ya Wanawake nchini (KWPL) kimemsajili nahodha wa Harambee Starlets, Dorcas Shikobe kadri kinavyozidi kujisuka upya kwa minajili ya kampeni za msimu ujao wa 2020-21.

Shikobe anaingia katika sajili rasmi ya Queens waliotawazwa mabingwa wa KWPL mnamo 2017 baada ya kuagana rasmi na Oserian Ladies waliojivunia huduma zake mnamo 2019. Ametia saini mkataba wa miaka mitatu.

Katika mahojiano yake na Taifa Leo, Fredrick Chege ambaye ni Meneja wa Queens amesema kwamba ujio wa Shikobe utaimarisha zaidi safu yao ya ulinzi na kuwapa kila sababu ya kutwaa taji la msimu huu wa KWPL utakaoanza rasmi mnamo Disemba 12.

“Shikobe ni miongoni mwa mabeki matata zaidi katika KWPL kwa sasa. Shikobe analeta tajriba pevu itakayotukweza pazuri. Tatizo letu limekuwa kwenye idara ya ulinzi ambayo kwa sasa imepigwa jeki pakubwa,” akasema Chege.

Shikobe anaingia kambini mwa Queens baada ya uhamisho hadi Yanga Princess ya Tanzania kugonga ukuta.

“Yanga walitarajiwa kunipokeza kima cha Sh100,000 za kutia saini mkataba. Walitazamiwa pia kulipa ada ya Sh200,000 za uhamisho. Lakini badala yake, walisema wangenipa Sh50,000 pekee kisha kukamilisha salio baadaye,” akasema Shikobe.

Kwa kuingia Queens, Shikobe anarejea katika kikosi alichoagana nacho kabla ya kuingia Oserian mnamo 2015.

Thika Queens wameratibiwa kufungua kampeni zao za KWPL msimu ujao dhidi ya limbukeni wa ligi hiyo, Ulinzi Starlets.