HabariSiasa

Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Maasai Mara kikaangoni

September 3rd, 2019 2 min read

Na WANDERI KAMAU

CHAMA cha Wafanyakazi wa Vyuo Vikuu Kenya (KUSU) kinamtaka Naibu Chansela wa Chuo Kikuu cha Maasai Mara Prof Mary Walingo kujiuzulu kutokana na madai ya ufujaji wa mamilioni ya pesa.

Madai hayo yalifichuliwa na taarifa ya kipekuzi iliyopeperushwa na runinga ya Citizen mnamo Jumapili, ambapo inadaiwa kuwa zaidi ya Sh190 milioni zilifujwa kwa maagizo ya msimamizi huyo tangu mwaka 2016.

Kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi jana, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt Charles Mukwaya alisema kuwa mkuu huyo anapaswa kujiondoa ili kuruhusu uchunguzi kuendelea au ashurutishwe kujiondoa na asasi za serikali.

“Tunamtaka Prof Walingo kujiuzulu ili kutoa nafasi ya uchunguzi kamili kuhusu madai hayo. Lazima ajiondoe ili kuwapa nafasi asasi husika nafasi ya kuendesha uchunguzi wao bila vikwazo vyovyote,” akasema Dkt Mukwaya.

Mnamo Jumatatu, maafisa kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) walifika katika chuo tayari kuanza uchunguzi wao. Kulingana na DCI, baadhi ya wafanyakazi tayari wameandikisha taarifa kuhusiana na sakata hiyo.

Chama pia kiliziomba idara za usalama kuimarisha ulinzi wa wafanyakazi waliofichua kashfa hiyo, wakisema kuwa huenda wakaanza kupokea vitisho.

“Ufichuzi huo umefanywa na wafanyakazi wa ngazi za chini chuoni, hivyo lazima serikali iwahakikishie usalama wao kwani kuna uwezekano kuwa watatishiwa na watu wanaodaiwa kuhusika katika sakata hiyo,” akasema.

Chama hicho vilevile kiliiomba serikali kutoangazia chuo hicho pekee, bali vyuo vyote vya umma nchini, ili kurejesha hali ya uwajibikaji, hasa usimamizi na matumizi ya fedha zinazotengewa.

Kilidai kuwa kimelalamikia usimamizi na matumizi ya pesa katika vyuo vikuu vya Masinde Muliro, Embu kati ya vingine.

Kulingana na ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, chuo hicho hakikueleza vile kilitumia Sh16.8 milioni za wanafunzi 494 licha ya kutowajumuisha kwenye sajili rasmi ya wanafunzi wake katika mwaka wa matumizi ya fedha za serikali wa 2015/206.

Chuo vile vile kilikosa kueleza kilivyotumia Sh12 milioni za mikopo ya wanafunzi, kwani kilipokea Sh72 milioni kutoka kwa Bodi ya Elimu ya Juu (HELB) licha ya kuomba Sh60 milioni.

Kwenye mojawapo ya video zilizorekodiwa kisiri, mkuu huyo anasikika akiwatishia wafanyakazi wake kwamba “watazama naye ikiwa ataenda gerezani.”