Naibu chifu afumaniwa akishiriki ngono na mwanafunzi

Naibu chifu afumaniwa akishiriki ngono na mwanafunzi

Na BRIAN OJAMAA

WANANCHI wenye ghadhabu katika soko la Cheptais, eneobunge la Mlima Elgon, Kaunti ya Bungoma, nusura wamchome naibu wa chifu baada ya kupatikana gesti na mwanafunzi wa Kidato cha Pili.

Wenyeji walifahamishwa kuhusu tukio hilo na mmiliki wa chumba cha malazi wawili hao walimokuwa, baada ya kushuku msichana huyo alikuwa mwanafunzi.

Mshukiwa alitambuliwa kama Bw James Jabunjey, ambaye ni naibu chifu wa Kata Ndogo ya Sasur.

Mwanafunzi huyo anasomea katika Shule ya Upili ya Toroso. Wawili hao walipatikana katika chumba cha malazi cha Kikwetu, kilicho katika mji wa Cheptais.

Baada ya kufahamishwa, wananchi walivamia chumba hicho na kumfurusha naibu chifu nje pamoja na msichana huyo.

Hata hivyo, polisi kutoka Kituo cha Polisi cha Cheptais walifika kwa haraka na kumwokoa chifu. Kamanda wa Polisi katika Kaunti Ndogo ya Mtlima Elgon, Stephen Muoni alithibitisha kisa hicho.

Alisema walifika hapo mara moja na kumkamata mshukiwa na msichana. Alisema kuwa baada ya kuwahoji wawili hao, ilibainika mshukiwa ni afisa wa serikali.

“Tumeanza uchunguzi kuhusu kisa hiki. Tutamfikisha mshukiwa mahakamani mara tu tutakapomaliza uchunguzi,” akasema.

Mkuu huyo alisema kuwa wanatuhumu mshukiwa ana uhusiano wa kimapenzi na msichana huyo.

“Ningetaka kuwaonya wananchi wanaowaharibu wasichana wachanga kwamba siku zao zimehesabiwa. Tutawakamata na kuhakikisha wamefungwa gerezani,” akasema.

Afisa anayesimamia masuala ya watoto katika Katika Kaunti Ndogo ya Cheptais, Bw Henry Bigoro, alisema wanafuatilia kisa hicho na watahakikisha haki imetendeka.

“Tumehakikisha mshukiwa amekamatwa. Ripoti za matibabu zimeonyesha msichana alishiriki ngono,” akasema. Alieleza wanangoja kupewa cheti cha kuzaliwa cha msichana ili kubaini umri wake.

Mwenyekiti wa Chama cha Maendeleo ya Wanawake (MYW) katika eneo hilo, Bi Eunice Chepchumba, alikashifu vikali kisa hicho huku akiapa kuhakikisha kukifuatilia hadi mwisho.

You can share this post!

Ogallo aapa kufukuzia kuwa Mkenya wa kwanza kushiriki Grand...

Presha Jubilee ilipe deni la Kalembe Ndile kabla ya mazishi...