Naibu Gavana wa Kericho Susan Kikwai afariki kutokana na corona

Naibu Gavana wa Kericho Susan Kikwai afariki kutokana na corona

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Gavana wa Kericho Susan Kikwai amefariki kutokana na ugonjwa wa Covid-19 katika hospitali ya Siloam, mjini Kericho.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na familia yake Jumamosi, marehemu alikuwa amelazwa katika kitengo cha kuwahudumia wagonjwa mahututi (ICU) katika hospitali hiyo tangu wiki jana.

“Aliondoka hospitalini Alhamisi lakini hali yake ikawa mbaya Ijumaa usiku ndipo akarejeshwa hospitalini tena. Alifariki Jumamosi mwendo wa saa tatu na nusu asubuhi,” mtu wa familia yake akasema.

Bi Kikwai alikuwa akihudumu kwa muhula wa pili na wa mwisho baada ya kuchaguliwa mnamo 2013 pamoja na Gavana Paul Kiprono Chepkwony.

Alikuwa bintiye aliyekuwa Waziri Msaidizi katika utawala wa rais wa zamani Daniel Moi, William Kikwai. Mzee Kikwai alifariki mnamo Novemba mwaka jana.

Susan alihudumu kama Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji (KenInvest) kuanzia miaka ya 2005 hadi 2012 kabla ya kuingia siasa.

Marehemu ni afisa wa ngazi ya juu zaidi serikali kufariki kutokana ugonjwa huu hatari wa Covid-19 ambao maambukizi yake yameingia awamu ya tatu.

Mnamo Ijumaa ugonjwa huo uliangamiza Waziri wa Fedha wa Mandera Ibrahim Barrow Hassan.

You can share this post!

TZ YAPATA SULUHU BAADA YA POMBE

Kinara wa zamani wa EACC akana kuhusika katika sakata ya...