Makala

Naibu Gavana wa Lamu afichua siri ya kusalia mtiifu kwa Timamy

March 21st, 2024 3 min read

NA KALUME KAZUNGU

USHIRIKIANO mzuri wa kikazi kati ya Gavana wa Lamu Issa Abdalla Timamy na Naibu Gavana Raphael Munyua Ndung’u, umeepushia kaunti hiyo migogoro kama inayoshuhudiwa katika baadhi ya magatuzi nchini.

Huku kaunti nyingi zikishuhudia mizozo au ubabe kati ya magavana na manaibu wao, kwa Lamu hilo ni tofauti kabisa.

Lakini je, hilo limeafikiwa vipi?

Katika mahojiano na Taifa Leo mnamo Jumatano, Bw Munyua aliweka wazi kuwa kufaulu kwake katika kuendeleza uhusiano mwema na bosi wake, Bw Timamy, kunatokana na viongozi hao wawili kuweka kando ubinafsi na badala yake kuamua kuwafanyia kazi wananchi.

Bw Munyua alikiri yapo mengi ya kuwatofautisha viongozi lakini kwao wawili, wameafikia kuelekeza fikra na ajenda zao katika kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wa Lamu na kuhakikisha kaunti hiyo inasonga mbele kimaendeleo.

Kila wakati anaposimama jukwaani kuhutubia, Bw Timamy amekuwa akisisitiza haja ya viongozi,iwe ni yeye kama Gavana,Wabunge,Seneta,Mbunge Mwakilishi Wa Wanawake Lamu na madiwani,kudumisha ushirikiano na umoja katika utendakazi wao kwa manufaa ya wananchi Wa Lamu.

“Kama Gavana,nitahakikisha sisi viongozi wote wa eneo hili tunatembea pamoja katika mwelekeo sambamba. Tukifanya hivyo itakuwa rahisi kwa kaunti yetu kuafikia maendeleo ambayo ni manufaa kwa wananchi wapiga kura wa eneo hili,” akasema Bw Timamy.

Naye Bw Munyua aliendelea kufichua siri nyingine ya kuwaepushia migongano magavana, manaibu wao Na viongozi wengine nchini, akisema ni vyema viongozi hao kuwa wenye kujitia hamnazo katika yale yanayosemwa na wapinzani na hata baadhi ya vibaraka wa kisiasa.

Alisema yeye binafsi kama Munyua ametukanwa na kubandikwa majina ya kejeli, ikiwemo kuitwa ‘Msichana wa Maua’ yaani ‘flower girl’.

“Hata waniite ‘Msichana wa Maua,’ ‘Mpambe wa Afisi ya Gavana’ na majina mengine, mimi sishtuki wala kukasirika,” akasema Bw Munyua.

Aliongeza kwamba lengo ni kuchapa kazi na “bila shaka wananchi watatambua bidii na maendeleo tunayoafikia katika kaunti yetu”.

“Siwezi kuacha changamoto zinazokabili eneo hili, ikiwemo utovu wa usalama, umaskini, ukosefu wa miundomsingi, elimu na afya duni na pia mgao kidogo kutoka kwa serikali kuu kila mwaka,” akasema.

Alisema kiongozi mzuri ni yule badala ya kuvutana na wenzake, anafaa kuelekeza fikra zake kwa maendeleo bila kupoteza muda.

“Sisi tumeamua kuweka kando tofauti za aina yoyote na kuhudumia wananchi wetu kikamilifu,” akasema.

Aliwataja wale viongozi wanaotumia muda mwingi kutofautiana na hata kuendeleza vita vya ubabe kati yao kuwa wabinafsi.

“Endapo tutaondoa ubinafsi na kushughulikia vilivyo wananchi waliotuchagua, sidhani tunaweza kushuhudia hivi vita vya kila mara kati ya magavana na manaibu wao nchini,” akasema.

Aliongeza kwamba punde kiongozi anapokuwa mbinafsi ndipo anapoanza kutaka makuu, “eti eeh, sijawekewa chai kwa afisi yangu, eeh, mgao wa kukimu afisi yangu wafaa uongezwe”.

Ikumbukwe kuwa naibu huyo wa gavana ni Mkristo huku Bw Timamy akiwa Mwislamu.

 

Bw Munyua Munyua Ndung’u (kushoto) akiwa na Gavana Issa Timamy. PICHA | KALUME KAZUNGU

Bw Munyua alishikilia kuwa sababu nyingine inayowafanya viongozi hao wawili kuendelea kushirikiana bila kuonyesha tofauti zao ni harakati za kuhakikisha wanaunganisha jamii na dini zote zipatikanazo Lamu.

Lamu ni kaunti ambayo ndani yanaishi karibu makabila yote zaidi ya 42 ya Kenya.

“Gavana wangu ni Mwislamu na mimi ni Mkristo. Twajitahidi kuwa kielelezo chema kwa wananchi,” akasisitiza Bw Munyua.

Baadhi ya wakazi wa Lamu waliohojiwa na Taifa Leo walikiri kupendezwa na uwiano mwema wanaodhihirisha gavana na naibu wake kila kuchao.

Bi Lucy Karani alisema endapo viongozi wote, hasa magavana na manaibu wao nchini wataiga mfano wa Bw Timamy na Bw Munyua na kuonyesha utumishi na heshima, utata wa pande hizo mbili utazikwa kwa kaburi la sahau.

“Inasikitisha kuona baadhi ya kaunti zikikosa kusonga mbele kimaendeleo kutokana na tofauti au vita baridi na wazi kati ya magavana na manaibu wao,” akasema Bi Karani, akiongeza kwamba mfano wa Bw Timamy na Bw Munyua unawasukuma hata nao wananchi kusalia kitu kimoja na kuzingatia amani, uwiano na utangangamano bila kujali huyu ni kabila gani au dini gani.

Bw Ahmed Yusuf naye aliwataka wakazi wa Lamu pia kuiga mfano wa Bw Timamy na Bw Munyua kwa kuhakikisha wanaheshimiana, kushirikiana, kutangamana na kutagusana bila ubaguzi wa kabila, dini au aina yoyote ya ulinganuo.

Bw Munyua alizaliwa eneo la Umoja, tarafa ya Mpeketoni, Lamu Magharibi.

Alisomea Shule ya Msingi ya Umoja kabla ya kujiunga na Shule ya Sekondari ya Mpeketoni.

Baadaye alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta alikosomea somo la hesabu zinazohusu usanifu mijengo na miradi mingine, yaani Architectural Mathematics.

Amewahi kufanya kazi na mashirika mbalimbali yasiyokuwa ya kiserikali hapa Kenya na pia nchi jirani ya Tanzania kabla ya kujiunga na siasa mnamo mwaka 2013, akiwa mgombea mwenza wa gavana wa zamani wa Lamu, Fahim Yasin Twaha.

Amewahi kuhudumu kama Waziri wa Afya wa Kaunti ya Lamu.

Mnamo 2022, alivuka na kuwa mgombea mwenza wa gavana wa sasa, Issa Timamy, muungano ambao ulimshinda Bw Twaha kwenye uchaguzi wa Agosti 9, 2022.

Bw Munyua ni baba wa watoto wawili.