Naibu Rais alenga kuwarai mabwanyenye wa Mzee Moi wamuunge mkono

Naibu Rais alenga kuwarai mabwanyenye wa Mzee Moi wamuunge mkono

Na ONYANGO K’ONYANGO

NAIBU Rais Dkt William Ruto sasa analenga kuwarai mabwanyenye na wandani wa aliyekuwa Rais, marehemu Daniel Arap Moi kutoka Bonde la Ufa, ili wamuunge mkono kuelekea uchaguzi wa 2022.

Mbinu hii kulingana na wandani wake pia inalenga kufifisha umaarufu wa hasimu wake Gideon Moi ambaye ni mwanawe marehemu Mzee Moi.

Kati ya wale ambao Dkt Ruto analenga kuwafikia ni aliyekuwa Katibu wa Idara ya Mawasiliano ya Mzee Moi, Lee Njiru, mfanyabiashara tajiri, Joshua Kulei, mawaziri wa zamani Henry Kosgei na Franklin Bett, bwanyenye na aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara mbalimbali Benjamin Sogomo na mhubiri wa Mzee Moi, Silas Yego.

Lengo kuu la Dkt Ruto ni kuvunja himaya ya matajiri waliomzunguka Mzee Moi ili kuhakikisha kuwa hawamuungi mwanawe Bw Moi ambaye pia ni Seneta wa Baringo.

Inaaminika kuwa Ikulu inampendelea Bw Moi kurithi kiti hicho kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2022 na mrengo wa Dkt Ruto unalenga kumsawiri kama kiongozi asiyekuwa na umaarufu wowote.

Bw Njiru alikutana na Naibu Rais mnamo Disemba mwaka jana ambako inaaminika alishawishiwa awafikie baadhi ya waliokuwa wandani wa Mzee Moi ili kuhakikisha anadhibiti kura za Bonde la Ufa.

“Tunataka kuhakikisha kuwa Bw Moi anasalia na Mbunge wa Tiaty William Kamket pekee katika kambi yake na Katibu wa Kanu Nick Salat. Lengo letu ni kuhakikisha udhibiti wa kisiasa hapa Bonde la Ufa,” akasema Mbunge mmoja mwandani wa Dkt Ruto ambaye hakutaka jina lake linukuliwe.

Mbunge wa Soy Caleb Kositany alisema wanalenga kuvumisha Urais wa Dkt Ruto mashinani maeneo yote ya Bonde la Ufa ili kuhakikisha jamii yote ya Kalenjin iko nyuma yake.

“Tunalenga kuwavutia wote waliokuwa wakishirikiana na Mzee Moi upande wetu. Lee Njiru ambaye yupo katika kambi yetu ana tajiriba ya miaka mingi kisiasa na atatusaidia hata tunaposaka kura maeneo mengine,” akasema Bw Kositany.

Hata hivyo, mbunge wa Keiyo Kusini Daniel Rono na mwenzake wa Kapseret Oscar Sudi walidai kuwa ni mabwanyenye hao ambao wamekuwa wakimtafuta Dkt Ruto.

Mbunge wa Aldai Cornelius Serem pia anashikilia wazo hilo hilo, akisema mawimbi ya kisiasa ya Dkt Ruto yanavuma kotekote bondeni.“Ndiyo wamejiunga nasi kwa sababu hawana njia nyingine. Huwezi kulinganisha umaarufu wa Ruto na Moi hapa Bonde la Ufa,’ akasema Bw Sudi.

Hata hivyo, Mabw Bett, Yego na Sogomo walisema kuwa hawajafikiwa na mrengo wowote uwe wa Dkt Ruto au Seneta Moi.? ‘Mrengo wowote haujanifikia kuhusu 2022.

Nitafanya uamuzi wa mwaniaji wa kuunga 2022 baadaye lakini wote ni viongozi wetu,’ akasema Bw Sogomo.? Bw Bett alifichua kwamba amekuwa akikutana na Seneta Moi lakini hawajajadili chochote kuhusu siasa za uchaguzi wa 2022.

‘Nilikuwa na uhusiano wa karibu na Mzee Moi na watoto wake ndiyo maana bado mimi hukutana na Gideon. Upande wa Ruto pia haujanifikia na nitafanya uamuzi baada ya kutathmini masuala kadhaa kati ya wawili hao,’ akasema Bw Bett.? Bw Salat naye alifichua kuwa pia wao wanataka kudumisha himaya ya Mzee Moi na kusalia na viongozi waliomsaidia wakati wa uongozi wake wa miaka 24.

You can share this post!

Uhuru atupa marafiki

Rais Suluhu aachilia huru wafungwa 5,001