Michezo

Nairobi City Stars yakamilisha usajili wa Rowland Makati

August 19th, 2020 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

KLABU ya Nairobi City Stars imekamilisha usajili wa kiungo Rowland Makati kwa mkataba wa muda mrefu.

Kijana huyo mwenye umri wa miaka 19 aliisaidia Dagoretti Mixed kutwaa ubingwa Chapa Dimba wa jimbo la Nairobi michuano hiyo ilipofanyika katika shule ya Jamhuri High mwezi Februari 2020; wakati huo akichezea timu ya Vapor Sports FC ya Daraja la Kwanza.

Akizungmza baada ya kupata habati hizo, nyota huyo alisema amefurahia kupewa nafasi ya kucheza katika Ligi Kuu ya Kenya (KPL) baada ya ndoto za muda mrefu.

Mshirikishi wa City Stars, Samson Otieno alisema kijana huyo alionekana wakati wa mashindano ya Chapa Dimba ambapo tangu wakati huo amekuwa kwenye rada ya City Stars hata wakati huu shughuli za michezo zimesimama kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

“Tumempata kutoka timu yetu ya kunoa vijana ya Vapor Sports ambapo amekuwa miongoni mwa wengine wasiozidi umri wa miaka 20 ambao baadaye watapata nafasi ya kujiunga na timu kuu ya City watakaporidhisha idara yetu ya kiufundi.”

Kinda huyo anayemiliki vyema nambari 10 amepewa jezi nambari 14 katika klabu hiyo yake mpya.