Michezo

Nairobi City Stars yazidi kutesa kipute cha BNSL msimu huu

January 28th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

MCHEZAJI Davis Agesa alipiga kombora moja la kiuhakika na kubeba Nairobi City Stars maarufu Simba wa Nairobi kuendelea kunguruma kwenye mechi za Betika Supa Ligi ya Taifa (BNSL).

City Stars ya kocha, Sanjin Alagin ilitia kapuni pointi tatu ilipobugiza Vihiga United bao 1-0 kwenye patashika iliyopigwa Mumias Sports Complex mjini humo.

Nayo Bidco United ingali mbili bora ilipolaza FC Talanta bao 1-0 kupitia Eric Gichimu huku Ushuru ikichapa Administration Police (AP) 3-1 na kutinga nne bora.

Agesa alifunga dakika ya 38 kufuatia pasi ya Oliver Maloba na kuashiria hataki mzaha.

Naye kipa Opiyo ‘Levis’ Lovae wa City Stars aliibuka shujaa alipopangua penalti baada ya Elvis Ojiambo kuangushwa ndani ya kijisanduku.

”Tunashukuru Mola kwa neema yake alitusaidia kuendeleza kusudio letu msimu huu,” alisema kocha wa City Stars.

APs Bomet iligeuka maembe mbele ya Nairobi Stima iliyowazidi ujanja na kuinyuka mabao 3-0 kupitia Patrick Mugendi aliyepiga kombora mbili huku Ronald Okello akiitingia bao moja.

Wachezaji wa Kenya Police walizoa alama moja baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Fortune Sacco lililofungwa na David Okiki dakika ya 66. Teddian Atuto aliiweka Fortune Sacco kifua mbele dakika ya 13.

Katika msimamo wa ngarambe hiyo, City Stars inaongoza kwa alama 52, saba mbele ya Bidco United baada ya kushuka dimbani mara 21 kila moja. Matokeo mengine, kibera Black Stars 3-1 St Josephs Youth, Shabana 0-1 Modern Coast Rangers, Vihiga Bullets 3-0 Murang’a Seal na Migori Youth 2-2 Coast Stima.