Habari Mseto

Nairobi kupata Naibu Gavana hivi karibuni

February 10th, 2020 2 min read

Na RICHARD MUNGUTI

HIVI karibuni kaunti ya Nairobi itakuwa na naibu wa Gavana baada ya tume huru ya uchaguzi na mipaka kuidhinisha uteuzi wa Ann Kananu Mwenda.

Bi Mwenda aliteuliwa na Gavana Mike Sonko Desemba 2019 baada ya kushtakiwa kwa ufujaji wa Sh357m za umma.

Uidhinishwaji wa Bi Mwenda unafuatia ufafanuzi wa Mahakama ya Juu kuwa haijatoa uamuzi wowote wa kufutilia mbali uteuzi wa Bi Mwenda.

Na wakati huo huo Mahakama hii ilisema kesi iliyowasilishwa na Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi, Bi Beatrice Elachi sio kizingiti cha kumzuia Gavana Sonko kutekeleza majukumu yake ya kikatiba.

Kupitia kwa naibu wa msajili wa Mahakama ya Juu Bw Daniel ole Keiwua, mahakama imeelezea kuwa haijasikiza kesi iliyowasilishwa na Bi Elachi akiomba ufafanuzi wa masuala kadhaa ya kikatiba kuhusu utenda kazi katika kaunti ya Nairobi bila Gavana.

Katika kesi iliyowasilishwa na Serikali ya Kaunti ya Nairobi na wakili John Diro, mahakama imeombwa ifafanue “iwapo Spika anaweza tekeleza majukumu ya Ugavana wa Nairobi wakati huu Bw Sonko ameshtakiwa na hakuna naibu wake.”

Mahakama hii ya upeo inaombwa ifafanue ikiwa masharti ya dhamana wanayopewa magavana wanaposhtakiwa yana maana kwamba “wameondolewa afisini.”

Jaji Mkuu David Maraga na majaji wa mahakama ya juu watafafanua ikiwa Gavana Sonko anaweza kumteua naibu wake kama “ hayuko afisini.”

Majaji hao wa mahakama ya juu watafafanua kile “Pia Spika anaomba mahakama ifafanue athari za kutochapishwa kwa jina la Polycap Igathe katika gazeti rasmi la Serikali alipojiuzulu.

Anahoji ikiwa Bw Igathe anaweza kutekeleza majukumu yake.

Hata hivyo Bw ole Keiwua amesema kuwa kesi hiyo sio kizingiti cha kumzuia Bw Sonko kutekeleza majukumu yake.

Naibu huyo wa msajili wa mahakama hii ya upeo amesema baada ya kesi hiyo kusikizwa uamuzi utakaofikiwa utachapishwa katika vyombo vya habari.

Mawakili Prof Tom Ojienda na Harrison Kinyanjui wanaowakilisha Bw Sonko na kaunti ya Nairobi wamedumisha msimamo wa kisheria kuwa “Sonko ndiye Gavana wa Kaunti ya Nairobi.”

Na wakati huo huo tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC imeidhinisha uteuzi wa naibu wa Gavana Ann Kananu Mwenda.

Kuidhinisgwa kwa Bi Mwenda kunaelekea kuondoa kizugumkuti cha usimamizi katika kaunti ya Nairobi.

Katika ufafanuzi uliotolewa, Bw Keiwua alikuwa ameeleza wazi kuwa kesi aliyowasilisha Spika sio kizingiti kwa idara yoyote ile kutekeleza jukumu lake la kikatiba.

Nakala ya ufafanuzi huo ilipelekewa mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati.