Habari Mseto

Nairobi na Nakuru zavuna zaidi katika pendekezo jipya la ugavi wa fedha za kaunti

September 18th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KAUNTI ya Nairobi ndiyo itapata nyongeza kubwa zaidi ya mgao wa fedha mwaka ujao mfumo mpya wa ugavi wa fedha baina ya kaunti utakapoanza kutumika.

Kaunti hiyo inayosimamiwa na Gavana Mike Sonko na Idara ya Huduma za Nairobi (NMS) itapokea Sh3.3 bilioni zaidi na hivyo kufikisha mgao wake kuwa Sh19 bilioni, kutoka Sh15.9 bilioni mwaka huu.

Itafuatwa kwa kaunti ya Nakuru ambayo itapata nyongeza ya Sh2.5 na hivyo mgao wake kutimu Sh13 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2021/2022.

Kiambu itapokea Sh2.2 bilioni zaidi na hivyo kupandisha mgao wake hadi Sh11.7 bilioni huku Turkana ikipata Sh2 bilioni zaidi ishara kuwa itapata jumla ya Sh12 bilioni, Kakamega (Sh1.9 bilioni zaidi), Bungoma (Sh1.7 bilioni), Uasin Gishu (Sh1.6 bilioni), Nandi (Sh1.5 bilioni), Kitui (Sh1.5 bilioni) na Kajiado (Sh1.4 bilioni).

Kaunti ambayo zitakapa nyongeza isiyo kubwa zaidi ni pamoja na; Tharaka Nithi ambayo itapata Sh289 milioni, Nyamira (Sh324 milioni), Vihiga (Sh414 milioni), Isiolo (Sh469 milioni), Kwale (Sh479 milioni) na Marsabit (Sh503 milioni).

Kaunti ya Lamu ambayo kila mwaka ndio hupata mgao wa chini zaidi sasa utapata nyongeza ya Sh510 milioni kuanzia mwaka ujao na hivyo kufikisha mgao wake kuwa Sh3.1 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2021/2022.

Chini ya mfumo huo ambao ulipitishwa na maseneta wote pasina aliyepinga, hakuna kaunti itakayopokea pesa kidogo kuliko zile ambazo ilipata katika mwaka jana na itapata mwaka huu.

Katika mwaka ujao kaunti zitarajia kupokea Sh370 bilioni baada ya serikali ya kitaifa kukubalia kuongeza Sh53.5 bilioni juu ya mgao wa mwaka huu wa Sh316.5 bilioni.