Michezo

Nairobi sasa kuwa na maabara ya kupima watumiaji pufya

August 27th, 2018 2 min read

Na Geoffrey Anene

Baada ya visa vya matumizi ya pufya kuongezeka nchini Kenya, zoezi la kupima utumiaji wa dawa za kusisimua misuli sasa limeletwa ‘mlangoni.’

Eneo la Afrika Mashariki sasa lina Maabara ya kiwango cha kimataifa ya kuchunguza utumiaji wa dawa za kusisimua misuli michezoni.

Maabara yenyewe yatakuwa jijini Nairobi. Yataanza kuhudumu mapema Septemba mwaka 2018.

Baada ya mradi wa miezi tisa ulioanzishwa na kufadhiliwa na Kitengo cha Uadilifu katika Riadha (AIU) kwa ushirikiano wa Wakfu wa Riadha, Maabara ya kampuni ya LANCET Group of Labs East Africa, ambayo yanahudumu kama Pathologists Lancet Kenya, yamefanikiwa katika ombi lao la maabara yao jijini Nairobi kuwa maabara yaliyoidhinishwa na Shirika la Kukabiliana na matumizi ya pufya duniani (WADA) kuchunguza damu ya wanariadha.

Mradi wa AIU ulipata ushauri wa kuchagua maabara katika eneo la Afrika Mashariki kutoka kwa idara ya Utafiti ya Sayansi ya Kukabiliana na Matumizi ya Pufya (REDs) katika Chuo Kikuu cha Lausanne nchini Uswizi na kisha kuandaa mafunzo na ushauri ya kufundi ili kufikia viwango vya kukubaliwa na WADA. Awamu ya kwanza ya mafunzo imekamilika, huku mafunzo yakitarajiwa kufanywa jinsi inavyotakikana.

Kuanzia mapema Septemba mwaka 2018, maabara haya ya Nairobi yatachunguza damu kusaidia mradi wa AIU wa kuweka uchunguzi wa kielekroniki wa kila mwanaspoti almaarufu “Athlete Biological Passport” pamoja na mipango mingine ya kukabiliana na uovu wa kutumia dawa haramu michezoni kama ile ya Shirika la Kukabiliana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli la Kenya (ADAK).

Kuwepo kwa maabara haya katika eneo la Afrika Mashariki, sampuli za damu sasa hazitahitajika kusafirishwa hadi maabara ya Bara Ulaya ama nchini Afrika Kusini kwa uchunguzi, AIU imesema Agosti 27, 2018.

Imefichua kwamba zoezi la kufanyia uchunguzi Afrika Kusini na Bara Ulaya lilikuwa ghali sana na lilikuwa na changamoto zake hasa za kuhakikisha vipimo hivyo vinafanywa kwa muda uliotengwa.

Tangu mwaka 2012, Kenya imeshuhudia zaidi ya wanariadha 50 wakipigwa marufuku kwa kupatikana wahalifu wa dawa hizo haramu. Mwezi huu wa Agosti umeshuhudia malkia wa zamani wa Jumuiya ya Madola wa mbio za mita 10, 000 Lucy Kabuu Wangui na chipukizi matata wa mbio za mita 800 Kipyegon Bett wakiingia katika orodha hiyo mbovu.