Michezo

Nairobi Water yajipanga kurejea ligini

July 21st, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

BAADA ya timu ya soka ya Nairobi Water kulemewa kufanya kweli kwenye mechi za Kundi A kuwania taji la Nairobi East Regional League (NERL) sasa inalenga kurejea kivingine kwenye kampeni za msimu ujao endapo itafadhiliwa.

Kikosi hicho kiliopania kutwaa ubingwa huo na kunasa tiketi ya kusonga mbele kushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Pili kilijikuta njiapanda baada ya kulemewa kuhimili makali ya wapinzani wao na kumaliza kati ya tano bora kwa kuzoa alama 27 sawa na FC Barca tofauti ikiwa idadi ya mabao.

Kocha wake, Ndung’u Ndichu anasema ”Mwanzo wa ngoma tunajiapanga kwa ajili ya kushiriki mashindano ya kila mwaka ya kampuni za maji kote nchini yatakayoandaliwa mjini Embu mwezi ujao.”

Alidai kwamba wamepania kutifua vumbi kali ili kuhifadhi taji la kipute hicho ambalo tangu mwaka 2012 walilipoteza mara moja mwaka 2016 walipomaliza nafasi tatu kwenye mechi zilizoandaliwa mjini Machakos.

Kisha alidokeza kwamba katika mpango mzima wamepania kuzungumza na wasimamizi wao ili kujadiliana kuhusu mipango ya msimu ujao. Hata hivyo alidai hawakutarajia matokeo kama hayo mbali walipania kumaliza katika nafasi ya kwanza na kutwaa tiketi ya kupandishwa ngazi msimu ujao.

”Baada ya kumaliza nafasi ya nne msimu wa 2018/2019 tayari msimu huu tulitarajia kufanya vizuri zaidi na kuibuka kileleni ili kusonga mbele muhula ujao,” alisema na kuongeza kwamba hata hawaamini kilichochangia vijana hao kuteleza na kushindwa kutimiza azimio hilo.

Kocha huyo hushirikiana na naibu wake Dennis Mambo kusukuma gurudumu la kikosi hicho ambacho asimilia kubwa ya wachezaji wake ni wafanyi kazi katika kampuni hiyo ya maji.

Nairobi Water ilikuwa miongoni mwa vikosi vilivyotifua kivumbi kikali kwenye kampeni za kuwania ubingwa huo lakini ilijikuta kwenye wakati mgumu ilipokutanishwa na baadhi ya mahasimu wakuu ikiwamo Mbotela Kamaliza na Uprising FC kati ya wengine.

Naibu huyo wa kocha, Dennis Mambo alisema “Tukirejea kushiriki mechi za Ligi msimu ujao tutalazimika kuongezea wachezaji wapya wenye ujuzi ili kuchochea wenzao angalau tufanye vizuri na kuosnga mbele.”

Nairobi Water inajumuisha: Obediah Nyabuto, Stanislaus Ywayo, Mohammed Kai, Phernandez Imbwaka, Brian Omondi, Peter Odoyo, Joseph Tonny, Joseph Ochung, Godrick Juma, Daniel Ochieng (nahodha), Daniel Nyambura, John Oliech, Fredrick Osambo, Elijah Sinei, Humphrey Obare, Simon Kariuki na Walter Odhiambo. Pia wapo Moses Augustino, Linus Nyongesa, Brian Otiato, Charles Okelo, Alex Orima, Hillary Kipchumba, Denis Muthini, Victor Kyalo, Kevin Were, Stephen Odhiambo, Fredrick Onzere na Ian Munene.