Michezo

Nakitare apiga Spitfire bao la uchungu kuinyanyua Butterfly

March 18th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

MCHEZAJI mahiri Evans Nakitare alifanikiwa kutikisa nyavu mara moja na kuibeba Butterfly FC kuishinda  Spitfire bao 1-0 kwenye mechi ya Kundi C Ligi ya Taifa Daraja la Pili iliyopigiwa uwanja wa Shule ya Msingi ya Ruiru.

Butterfly ilijiongezea alama tatu muhimu na kulipiza kisasi baada ya kuteleza na kupigwa mabao 3-2 na Gor Mahia Youth wiki iliyopita.

”Sina shaka kuwashuruku wanasoka wangu kwa kazi njema walioshusha pia nawahimiza kuendeleza mtindo huo kwenye mechi sijazo,” alisema kocha wa Butterfly Bernard Shikuri.

Nayo Gor Mahia Youth ilitoka nguvu sawa bao 1-1 na CMS Allstars huku Tandaza FC ikiyeyusha alama zote muhimu ilipolala kwa mabao 4-0 mbele ya Kibra United. Kwenye mechi hizo, Wajiji FC ilitandikwa mabao 3-1 na Gogo Boys kutokana na juhudi zake, Nobert Obasanjo aliyepiga kombora mbili safi huku Hillary Odhiambo akiitingia bao moja.

Nao Michael Kinywa na Benson ‘Roro’ Ngare kila mmoja aliangusha kombora zito kimiani na kusaidia Karatina Homeboys kuvuna mabao 2-1 dhidi ya Mku Thika. Nao wanasoka wa Mathaithi walishindwa kufana na kulazimisha sare tasa na Bomas of Kenya.

Kwenye mfululizo huo MKU Thika ilipokezwa pigo nyingine kabla ya kupona majeraha ya kupondwa mabao 3-2 na CMS Allstars wiki iliyopita.