Michezo

Nakumatt yanusia ligi kuu baada ya kulima Ushuru

October 19th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

NAKUMATT imepiga hatua kubwa katika juhudi zake za kusalia kwenye Ligi Kuu ya Soka ya Kenya baada ya kuchapa Ushuru 1-0 Oktoba 19 katika mechi ya mkondo wa kwanza ya kuamua nani kati yao atashiriki Ligi Kuu na Ligi ya Supa msimu ujao wa 2018-2019.

Tom Adwar alipachika bao hilo la ushindi katika dakika ya 20 kupitia frikiki murwa uwanjani Camp Toyoyo jijini Nairobi. Nakumatt, ambayo iliingia Ligi Kuu kwa mara ya kwanza kabisa mwaka 2017, ililinda bao lake kwa ujasiri hadi kipenga cha mwisho licha ya Ushuru kufanya mashambulizi makali kutafuta bao la kusawazisha.

Mechi hii hukutanisha timu iliyomaliza Ligi Kuu katika nafasi ya 16 na timu iliyokamilisha Ligi ya Supa katika nafasi ya tatu.

Mshindi kati ya Nakumatt na Ushuru baada ya mechi ya marudiano hapo Oktoba 28 atajikatia tiketi ya kushiriki Ligi Kuu msimu ujao, huku timu itakayoshindwa ishiriki Ligi ya Supa kushindania tiketi ya kuingia Ligi Kuu msimu 2019-2020. Mechi ya marudiano itasakatwa uwanjani Kasarani.

Western Stima na KCB zilimaliza Ligi ya Supa mwaka 2018 katika nafasi ya kwanza na pili na kupandishwa daraja moja kwa moja kushiriki Ligi Kuu. Ushuru ilikamilisha nyuma ya Stima na KCB na kulazimika kutafuta tiketi kwa kupambana na nambari 16 kutoka Ligi Kuu, Nakumatt.