WANDERI KAMAU: Ili kufikia hadhi iliyotwikwa, Nakuru iyaige majiji tajika duniani

WANDERI KAMAU: Ili kufikia hadhi iliyotwikwa, Nakuru iyaige majiji tajika duniani

Na WANDERI KAMAU 

HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta kuupandisha hadhi mji wa Nakuru kuwa jiji, inapaswa kuwa mwanzo wa vitendo kwa uongozi wa jiji hilo jipya kudhihirisha kwamba lilihitaji hadhi hiyo.

Sababu kuu ni kwamba, hapo awali tumeshuhudia taasisi muhimu zikipandishwa hadhi kwa mbwembwe na bashasha nyingi, ijapokuwa hatua hiyo hugeuka kuwa kosa kubwa la kimkakati.

Ni hatua ambazo baadaye huja kukosolewa na wadau mbalimbali, kwani wengi huwa hawashirikishwi ifaavyo wakati uamuzi huo unapofanywa.

Baadhi ya makosa yaliyoshuhudiwa hapo awali ni kupandishwa hadhi kwa baadhi ya taasisi za elimu kuwa vyuo vikuu ama vyuo vyenyewe kupewa barua za kuanza kutoa mafunzo ya kozi muhimu, bila kufikisha viwango vinavyohitajika.

Kosa kubwa ambalo hufanyika katika hatua hizi ni kwamba nyingi hutekelezwa kisiasa.

Wito

Kwa mfano, kumekuwa na vilio kutoka kwa kaunti mbalimbali nchini zikitaka “kupewa” vyuo vikuu na Serikali ya Kitaifa.

Swali ni je: Kaunti hizo zimejitayarisha kuwekeza katika taasisi husika ili kuzifikisha katika viwango vinavyohita ili kutawazwa vyuo vikuu?

Vivyo hivyo, hilo ndilo swali na changamoto kuu iliyopo kwa viongozi wanaoshikilia nyadhifa mbalimbali katika Kaunti ya Nakuru.

Je, watadumisha hadhi mpya ya jiji hilo? Wako tayari kuchukua hatua zitakazoliwezesha jiji hili kuwa miongoni mwa majiji yanayotajika duniani kama London, New York, Tokyo au Paris?

Wako tayari kuboresha utoaji huduma kwa wenyeji kuwiana na viwango vya kisasa?

Wako tayari kuanzisha ushirikiano na uongozi wa majiji hayo tajika kufikisha Nakuru katika viwango hivyo?

akamau@ke.nationmedia.com

  • Tags

You can share this post!

Ashtakiwa kwa kuiba Biblia

TAHARIRI: Mazimwi yanayokula soka yetu yazimwe

T L