Makala

NAKURU: Nyani wanaopokonya walevi pombe na kuiba chakula cha wakazi

January 10th, 2019 3 min read

NA RICHARD MAOSI

KATIKA mji wa Nakuru, mitaa imepewa majina yao kutokana na sifa zake au hali halisi ya maisha. Mojawapo ya maeneo hayo ni mtaa wa Manyani ambapo nyani na tumbili wamekuwa wageni bila mwaliko katika nyumba za watu.

Idadi kubwa ya nyani hufunga safari kutoka kwenye Mbuga ya Kitaifa ya Nakuru, wakielekea kwenye mashamba na makazi ya watu bila kuogopa chochote.

Mhudumu wa hoteli ya Summit, Nakuru afukuza nyani anaosema wamemhangaisha asijue la kufanya. Picha/ Richard Maosi

Wakati Taifa Leo Dijitali ilikita kambi eneo hili kupekua taarifa hizi kwa kina, tulikumbana na viumbe hawa wakiendelea na shughuli zao kama kawaida lakini walipogundua sisi si wenyeji walionekana kusitisha shughuli zao na kututazama.

Wakazi wengi wanasema wamekuwa na changamoto kuwakabili, lna juhudi zao za kuwaangamiza zimeambuli pakavu huku wakiomba usaidizi kutoka kwa serikali ya kaunti ambayo imefumbia macho janga hili.

Anasimulia hasara anayopata kutokana na uharibifu wa nyani. Hapa waliharibu meza inayotumiwa na watalii. Picha/ Richard Maosi

Mahangaiko

Waliokuwa wakiweka ulinzi mkali wa mbwa nao wamebadilisha mtindo walipogundua mbinu hiyo haisaidii, pale wanaposhambuliwa na kutiwa majeraha kutokana na kichapo cha kundi la nyani usiku.

Dickens Ngota anasema amekuwa akiishi hapa kwa miezi sita. Anaungama kuwa wakazi wanafaa kujilaumu kwani wao ndio waliamua kuwakaribisha kwa maisha yao ya kibinafsi kwa dhana kuwa wangekuwa marafiki.

Aidha nyani wanapokosa chakula msituni, huruka seng’enge iliyozunguka mbuga ya Nakuru na kuvunja nyumba za watu bila kujali wakitarajia kulishwa kwa lazima au kuiba.

Nyani huyu anasubiri duka lifunguliwe ndipo arushiwe vyakula vilivyoharibika ale. Picha/ Richard Maosi

“Wiki iliyopita nilimkuta nyani akitokea dirishani baada ya kuchukua mayai ya kuku wangu. Siku hizi uhalifu unatekelezwa na nyani ambao wamegeuka kuwa majambazi sugu, wakati mwingine hata wamekuwa wakiwapokonya watoto vitabu wanapotoka shuleni,” alisema.

Tony Mogaka alisema nyani hawaogopi wanawake, na ndio sababu wanapenda kuzuru makazi yanayolindwa na akina mama.

“Wanawake wamekuwa wakiwabembeleza, kuwapa chakula na kuwakaribisha nyumbani na hii ndiyo sababu kuwatimua itakuwa ni kazi ngumu,” Tony alisema.

Binti huyu anamvizia nyani huyu ili ampige kumtorosha aende mbali na ploti anapoishi. Picha/ Richard Maosi

Wanapenda mlo

Wameendeleza tabia ya kuteka mali peupe na kuwapokonya wakazi vitu kama vile mkate na maziwa wakitoka dukani. Wengine hufika katika boma za watu wakiwa wamebeba mikebe ya kutiliwa chakula.

Betty Maina anasema alilazimika kuhama mtaa wa Manyani hadi Free Area kwa sababu siku moja kundi la tumbili lilimvamia jikoni na kubeba unga wote alipokuwa akitaka kuandalia familia yake chakula cha jioni baada ya kazi.

Nyani akila maganda ya ndizi na vyakula vilivyotupwa kando ya barabara. Picha/ Richard Maosi

“Hawa wanyama¬† hawana adabu hata kidogo wamekuwa kizingiti kikubwa cha maendeleo, hata sijui walitoka dunia gani,” alilalama.

Kitoweo cha nyama choma barabarani sasa ni maarufu katika mtaa wa Manyani baada ya mtindo wa nyani kuuawa na wakazi kisha kuliwa kuongezeka.

Lakini wafanyibiashara kwa hakika wanaendelea kujipatia hela za haraka na kuwavutia wateja wengi wanaomiminika kila siku vibandani kula mutura wa bei nafuu.

Mwanamume ategea kuwapiga nyani hawa. Picha/ Richard Maosi

Nyama ya nyani

Inahofiwa wengi wa wakazi hapa wamekuwa wakiburudika kwa nyama ya nyani au tumbili bila kujua huku maswali mengi kuliko majibu yakiibuliwa kwa walinzi wa mbuga endapo wamekuwa wakishika doria.

“Mchana utawakuta nyani wameshinda na watu lakini baadaye wanatoweka bila kujulikana wameenda wapi,” alitufichulia Dan Misik .

Wanawake wamelaumiwa sana kwa kuwabembeleza nyani kwa kuwarushia vyakula. Picha/ Richard Maosi

Wakazi hapa walikoma kula nyama za mutura njiani baada ya kukuta mizoga vichakani inayoshukiwa imekuwa ikitumika kuandaa nyama na supu.

Walevi kwa upande mwingine wamelalamikia taabu wanazopata mikononi mwa nyani.

Baadhi yao huhofia kurejea nyumbani wakiwa wamechelewa wakiogopa kushambuliwa na kucharazwa na nyani wanaowasubiri njiani.

Nyani hawa wanajua kukwea ukuta na kuingia kwa ploti za wakazi Nakuru. Picha/ Richard Maosi

Kupokonya walevi pombe

Erick Sule anasema alilazimika kukomesha mwenendo wa kubugia vileo jeshi la nyani lilipompokonya chupa ya bia usiku wa kuamkia mwaka mpya.

“Walinifuata hadi karibu na nyumba yangu kisha wakachukua bia niliyokuwa nimenunuliwa na rafiki yangu. Wakaanza kugawana wakikimbilia usalama wao mbugani nilipotaka kuwatia adabu!” alisimulia.

Nyani ajituliza juu ya nyumba mtaani Manyani, Nakuru. Picha/ Richard Maosi

Wanyama hawa pia hawajawaogopa wanabodaboda ambao wanakiri biashara yao imevurugwa sana huku wakati mwingine wakienda na funguo za pikipiki.

“Majuzi niliacha ufunguo kwa pikipiki yangu. Niliporudi nikataka kuiwasha nihudumie mteja, nilipata nyani mmoja amechukua ufunguo huo na kuukatalia. Sasa ilinibidi nimbembeleze anipe lakini wakati mwingine wao hukataa na kutokomea msituni,” anasimulia Gabriel Kiptoo ambaye ni mwanabodaboda eneo hili. https://videospelautomater.com/svenska-casinon/casinoheroes.html

Mtaa wa Manyani unapakana na mbuga ya Nakuru katika sehemu ya Kusini ambapo nyani hawa huingilia na kuwacha wakazi wakilia hoi.

Nyani wakiharibu paa ya nyumba ili wajitome ndani wabebe vyakula. Picha/ Richard Maosi

“Nyani na wanyama wengine wamekuwa wakivuka uzio na kuingia mitaani Kaptembwa, Shaabab, Rhonda na Free Area. Hata uweke ulinzi namna gani, bado watavuka ua,” Sule alieleza.

Hata hivyo, walinzi wa mbuga wanawalaumu wakazi kwa kuwalisha nyani, licha ya marufuku kutoka kwa Wizara ya Utalii.

Kila unapokaribia mbuga ya Nakuru utaona mabango yaliyoandikwa ‘Usimpe Nyani Chakula’.

Nyani huyu anavuka ua wa umeme kwa kuruka kutoka mbugani hadi makazi ya watu. Picha/ Richard Maosi

Lakini raia wamekuwa wakipuuza ilani hii na kuwarushia maganda ya ndizi na mabaki ya chakula mita chache karibu na mbuga jambo linalowakaribisha mitaani.

Naibu Kaunti Kamishna wa Kaunti ya Nakuru Bw Herman Shambi alisema wakazi ni wa kulaumu kwani ndio huwapatia nyani chakula na kuwavutia kutoka mbugani.

“Ni lazima wakazi wakomeshe tabia ya kuwapatia nyani njugu na ndizi sokoni endapo wanataka kupunguza kero la nyani mitaani,” alisema.