Michezo

Nakuru West Queens waapa kuzima wapinzani KWPL

September 15th, 2019 2 min read

NA RICHARD MAOSI

Huu ni msimu mwingine mzuri kwa kikosi cha Nakuru West Queens ,timu ya akina dada inayofanya vyema katika ligi ya divisheni ya pili almaarufu kama supa.

Nakuru Queens sasa wamejiunga na ligi ya akina dada nchini KWPL (Kenya Women Premier League) na wametoa ahadi kuwa watatumia zana zao kuangamiza wapinzani.

Mkufunzi Benson Peters Esitoko anasema kuwa juhudi za wachezaji wake wapatao 50 ndio kichocheo kikubwa kwa mafanikio ya timu.

Alielezea Dimba kuwa haoni haja ya kutafuta vipaji vya soka kutoka kaunti nyinginezo nchini ilhali vipawa vimejaa katika kaunti ya Nakuru.

Alieleza kuwa Nakuru imekuwa ikichangia hazina ya vipaji katika ulingo wa soa kama vile Enosh Ochieng wa Ulinzi Stars aliyeibuka kuwa mfungaji bora 2019 KPL.

Kikosi hiki hushiriki mechi za nyumbani katika uwanja wa Afraha Stadium au Liberty, na ijapo kila siku za wiki wao hufanya mazoezi kwenye uga wa Shabbab unaopatikana viungani mwa mji wa Nakuru .

Kufikia sasa wanaongoza jedwali,kutokana na bidii zao kusajili ushindi mwingi katika jumla ya ligi ya supa ambayo ina ushindani mkali hasa wakati huu timu zote zinapopigania nafasi ya kushiriki KWPL mwakani.

Nakuru Queens imewasaidia akina dada wanaotokea katika familia za kimasini mitaani kujiepusha na swala la mihadarati na mimba za mapema.

Aidha wachezaji wamepiga hatua kubwa baadhi yao wakijikuta kwenye timu za haiba kubwa nchini kwa kutandaza kabumbu safi katika michuano yote wanayoshiriki.

“Mara ya kwanza nilikuwa na wakati mgumu kuwashawishi wazazi kunipatia watoto wao ikizingatiwa hii ni mitaa ya mabanda ambapo wengi wao hawaamini kuwa soka inaweza kulipa,” Peters akasema.

Lakini kadri ya muda ulivoanza kusonga baadhi yao waliona haja ya kuwaruhusu watoto wao kufuata ndoto zao.

Kufikia sasa kikosi hiki kilichoanzishwa zaidi ya miaka kumi iliyopita na wachezaji 10 tu ,kimefikisha zaidi ya wachezaji 50 wote wakipigania nafasi kujaza kikosi cha kwanza.

Timu yenyewe inashirikisha wachezaji baina ya miaka 16-22 na imefanikiwa kupata mashabiki wengi ambao humiminika kila siku za wiki kushuhudia wakipiga zoezi.

Mchezaji Stella Anyango na Zippora Magige ni miongoni mwa nyota wake ambao wanachezea kikosi cha timu ya Taifa Harambe Starlets chini ya miaka 22.

Anyango pia kwa misimu mitatu mtawalia amekuwa akiibuka kuwa mfungaji bora akitia kimyani zaidi ya magoli 23 kila msimu.

Jambo hili lilifanya avutie waajiri wapya kutoka Afrika kusini Banyana Banyana wanaohemea kupata huduma zake.

Anyango anasema anapania kufanya soka kama taaluma yake siku za mbeleni akiamini kuwa kipaji kinaweza kumfikisha mtu mbali muradi awe ana nia ya kutimiza ndoto yake.

Kile mchezaji anayejiunga na timu ya Quueens hubadilisha mienendo yake na kuipatia jamii mtazamo mpya kuwa soka sio mchezo tu wa wanaume bali pia wanawae wanaweza kutamba.

Kutokana na kandanda wasichana wanaweza kujifundisha mambo mengi kama vile kutunza saa,kujiheshimu na kubadilisha maisha ya wenzao.

Mahasimu zao wa jadi ni timu ya Ravine Roses na ile ya Nakuru East lakini kila wakati wamejizatiti kuhakikisha wanaandikisha matokeo mazuri .

“Mtaa wa Shaabab una mazingira magumu kwa mtoto wa kike na ndio sababu tumeamua kutumia mpira kubadilisha maisha kwa baadhi yao ambao walikuwa wamekata tama na maisha kabisa,”Esitoko alisema.

Esitoko anasema kuwa wazazi wao pia wamekuwa mstari wa mbele kuwapongeza mabinti zao kila mara wanapofanya vyema katika ratiba za michuano ya ligi.