Habari Mseto

Nakuru yahofia wanaoenda haja wazi wataleta maradhi

November 12th, 2018 2 min read

Na MAGDALENE WANJA

WIZARA ya Afya ya serikali ya Kaunti ya Nakuru imeelezea masikitiko yake kuhusiana na idadi kubwa ya watu ambao wanaenda haja kubwa katika barabara kuu ya Nairobi-Nakuru-Eldoret.

Wizara imesema kuwa hatua hiyo huenda ikasababisha mkurupuko wa maradhi haswa katika Kaunti ya Nakuru.

Idadi ya watu ambao wamegeuza barabara hiyo kuwa choo licha ya kuwepo kwa kampeni dhidi ya kwenda haja vichakani iliyozinduliwa mnamo 2017 katika Kaunti ya Nakuru.

Kulingana na wizara ya afya, kugeuza vichaka kuwa choo kumechangia pakubwa katika ongezeko la maradhi ya kuhara na homa ya tumbo katika Kaunti ya Nakuru.

Kufikia sasa vijiji 328 vimethibitishwa kukomesha tabia ya kwenda haja msituni tangu kuzinduliwa kwa kampeni ya kuwataka watu kutumia vyoo badala ya kwenda haja vichakani.

Idara ya Afya ya Umma imefadhili kampeni hiyo kwa ushirikiano na wahisani wengineo.

Kampeni hiyo inalenga kuhakikisha kuwa kufikia 2020 kila familia itakuwa na choo na hakutakuwa hata mtu mmoja anayeenda haja kubwa vichakani.

Kulingana na mshirikishi wa kaunti wa shirika la Maji, Mazingira na Usafi (WASH), Bi Margaret Kuibita, watu wanaoenda haja kubwa barabarani bado ni changamoto.

“Serikali ya Kaunti haimiliki kipande chochote cha ardhi kando ya barabara hivyo ni vigumu kuwajengea vyoo wapiti njia ambao wanaenda haja kubwa kando ya barabara,” akasema.

Mradi utagharimu takribani Sh167 milioni ili kuhakikisha kuwa kila familia katika vijiji vyote 2,052 kwenye kaunti hiyo inakuwa na choo.

Wahisani wengine wanaofadhili mradi huo ni Amref, Benki ya Dunia, Afya Uzazi kati ya wafadhili wengineo.

Kulingana na Bi Kuibita, kuna aina mbalimbali za kwenda haja vichakani.

Baadhi ya vyoo vya shimo vinavyotumiwa katika baadhi ya familia ni vibovu hivyo havina tofauti na mtu anayeenda haja kubwa kichakani.

“Unaweza kuwa na choo lakini kinavuja na uchafu unaelekea vichakani au katika eneo la wazi,” akasema.

Alisema kuna baadhi ya familia zilizo na vyoo lakini hawavitumii na badala yake wanaenda haja vichakani au eneo lililo wazi.

“Ili kijiji kiweze kuidhinishwa kwamba wakazi wake wanatumia vyoo ni sharti kitimize matakwa mbalimbali. Kwanza ni sharti kila familia iwe na choo na vifaa vya kunawa mikono na eneo lifaalo la kuelekeza uchafu vyoo vinapojaa,“ akaongeza.

Baada ya kutimiza hayo, kijiji sasa kiunaruhusiwa kuweka bango kubwa la kuonyesha kuwa wakazi wa eneo hilo hawaendi haja vichakani.