Michezo

Nalenga kuvunja dhana potovu 'Wakenya hawana lao soka ya Afrika Kusini' – Anthony Akumu

May 12th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIUNGO matata wa Harambee Stars, Anthony ‘Teddy’ Akumu amesema analenga kutamba zaidi katika soka ya Afrika Kusini licha ya dhana potovu ya tangu jadi kwamba Wakenya hushindwa kung’aa katika Ligi Kuu ya taifa hilo (PSL).

Akihojiwa na Capital Sports katika kituo cha redio cha Capital FM, Akumu ambaye amewahi pia kuchezea Gor Mahia katika Ligi Kuu ya Kenya (KPL) alisema analenga kuvunja itikadi kwamba visu vya makali ya wanasoka wazawa wa humu nchini husenea sana kila wanapotua Afrika Kusini.

“Nimewahi kuzisikia hadithi za aina hiyo; kwamba Wakenya hushindwa kufaulu katika soka ya Afrika Kusini. Naamini kwamba kufanikiwa kwa mchezaji yeyote kitaaluma ni zao la bidii na nidhamu ya mtu binafsi. Nipo Afrika Kusini kutamba,” akasema Akumu ambaye kwa sasa ni sogora wa Kaizer Chiefs.

Akumu anashikilia kwamba kubwa zaidi katika maazimio yake ni kusajili matokeo ya kuridhisha zaidi kuliko jinsi alivyofanya kambini mwa Zesco United nchini Zambia.

Aidha, amempongeza mwanasoka mwenzake katika timu ya taifa ya Harambee Stars, Brian Mandela kwa kumsaidia kuzoea haraka mazingira ya Afrika Kusini.

“Nimejitolea kujiimarisha zaidi ya nilivyofanya Zesco na kukabiliana vilivyo na changamoto mpya zilizopo mbele yangu katika Ligi Kuu ya PSL ambayo ni miongoni mwa vipute haiba kubwa zaidi katika soka ya bara la Afrika,” akasema Akumu.

Akumu ambaye pia amewahi kuwachezea Al-Khartoum FC nchini Sudan, aliingia katika sajili rasmi ya Kaizer Chiefs nchini Afrika Kusini mnamo Januari 2020 baada ya kuvunja ndoa yake na Zesco United ambao pia wanawapa hifadhi Wakenya David ‘Calabar’ Owino na Jesse Jackson Were.