Habari MsetoSiasa

Nambari ya Serikali ya kuripoti coronavirus yageuka 'mteja' bungeni

March 11th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WAZIRI wa Afya Mutahi Kagwe Jumatano jioni alikuwa na wakati mgumu kuelezea ni kwa nini wizara yake ilitoa nambari ya simu ya dharura (Hotline) kwa Wakenya, ya kutuma kutoa habari kuhusu maradhi ya coronavirus, ambayo haifanyi kazi.

Bw Kagwe alikuwa amefika mbele ya kamati ya pamoja ya bunge la kitaifa na seneti kuhusu afya kutoa maelezo kuhusu mikakati ambayo serikali imeweka kuzuia kutokea kwa maambukizi ya ugonjwa huo hatari.

Hii ni baada ya mwenyekiti wa kamati ya bunge la kitaifa kuhusu afya Bi Sabina Chege kujaribu kupifa nambari hiyo 0800721316 lakini ikageuka kuwa “mteja”.

Hii ilipelekea wabunge kushangaa ikiwa Wizara ya Afya ilikuwa ikiwachezea shere Wakenya kwa kuwasambazia kwa simu zao nambari ya simu ya dharura isiyofanya kazi.

Nambari hiyo ilitumiwa Wakenya kupitia ujumbe mfupi (SMS) kwenye simu zao wiki jana ili waweze kuripotisha visa wanavyoshuku kuwa vya maambukizi ya coronavirusi kwa Wizara ya Afya ili hatua za haraka zichukuliwe.

“Wizara inapasa kuwahakikishia Wakenya ikiwa nambari ya simu, ya dharura, isiyotozwa ada, ya 0800721316 iliyosambaziwa Wakenya inafanyakazi. Kwa sasa nimejaribu kuipiga na haijibiwi,” akasema Bi Chege.

Akijiitete wizara yake, Bw Kagwe alifafanua kwamba nambari hiyo ya simu ingali inafanyiwa majaribio na “hivyo karibu itaaza kufanya kazi bila hitilafu zozote”.

“Naomba radhi kwa mheshimiwa mwenyekiti umepiga nambari hiyo lakini haijajibiwa. Sababu ni kwamba bado tunaifanyia majaribio na pindi tutakapomaliza shughuli hiyo itaanza kufanya kazi sawasawa,” akasema.

Hata hivyo, Bw Kagwe hakueleza ni kwani nini Wizara yake iliwapa Wakenya nambari ya simu ambayo haikuwa imefanyika majaribio awali.

Hata hivyo, aliwaonya Wakenya dhidi ya kusambaza habari ambazo hazijadhibitishwa kupitia makundi ya mitandao ya kijamii kwani zinapotosha umma

“Kwa maelezo yoyote kuhusu ugonjwa wa COVID-19 tafadhali piga simu kwa Wizara ya Afya kupitia nambari za dharura zifuatazo: 0800721316, 0732353535, 0729471414,” Bw Kagwe akasema.

Waziri alipuuzilia mbali habari zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii kwamba Wizara inasaka watu wa kujitolea kutumiwa kufanya utafiti kuhusu COVID-19 kwa ada ya Sh400,000.

“Habari zinazosambazwa kwamba wanaume watakajitolea kufanyiwa utafiti kuhusu maradhi hayo watalipwa Sh400,000 ni za uwongo. Tunawahimiza Wakenya kutozingatia uvumi kama huo,” Bw Kagwe akasema.

Vile vile, alisema kuwa wageni wote wanaowasili nchini kutoka mataifa yote ya ulimwengu wanafanyiwa ukaguzi katika Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) kabla ya kuruhusiwa kutangamana na Wakenya.

“Kwa hivyo tuna maelezo ya abiria wote 239 waliwasili nchini kutoka jijini Wuhan, mkoa wa Huwei, China mwishoni mwa Februari na hawana virusi hivyo,” Bw Kagwe akasema.

Alikariri kuwa wanafunzi 100 raia wa Kenya walioko jijini Wuhan wako salama na serikali inaendelea kuwasaidia wakiwa huko.

“Hata wiki hii, tuliwatumia Sh10 milioni zaidi, pesa za matumizi. Hatuwezi kuwarejesha nchini kwani hiyo itahatarisha maisha yao hata zaidi,” Bw Kagwe akasema.