Nambari ya simu ‘ya Ruto’ yamulikwa ICC

Nambari ya simu ‘ya Ruto’ yamulikwa ICC

NA VALENTINE OBARA

UPANDE wa Mashtaka katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) umetetea vikali ushahidi wake kuwa nambari ya simu inayodaiwa kuwa ya Naibu Rais William Ruto, ni mojawapo ya ushahidi utakaothibitisha madai ya njama zilizotumiwa kuvuruga kesi ya ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007, iliyokuwa ikimkabili.

Katika taarifa za mwisho mahakamani kabla uamuzi utolewe kwenye kesi dhidi ya wakili Paul Gicheru, kiongozi wa mashtaka, Bw Anton Steynberg, Jumatatu alisisitiza kuwa wapelelezi walifanya uchunguzi wa kina kuhusu njama hizo.

Bw Gicheru, ambaye alihudhuria vikao vya Jumatatu kwa njia ya video, alidaiwa kuingilia kesi kwa njia iliyohujumu utendaji wa haki kupitia utoaji rushwa na kutumia vitisho dhidi ya mashahidi kwa niaba ya Dkt Ruto. Alikanusha mashtaka.

Kwa mujibu wa Bw Steynberg, ushahidi wote zikiwemo taarifa za mashahidi, rekodi za benki zinazodaiwa mashahidi waliweka mamilioni ya pesa walizohongwa na uchanganuzi wa mawasiliano ya simu, zimethibitisha Bw Gicheru ana hatia.

“Kuna ushahidi wa kutosha zikiwemo jumbe zilizotumwa kwa simu kutoka kwa benki kila wakati pesa zilipowekwa. Kuna hati za benki zilizo na majina ya mashahidi, sahihi za meneja wa benki na mihuri ya benki. Kuna takriban watu kumi waliotajwa katika kikundi cha njama za kumwokoa Ruto ambao wamehusishwa moja kwa moja na simu zilizopigiwa mashahidi,” akasema.

Uchunguzi

Aliongeza kuwa, uchunguzi wa kina wa ushahidi wa simu zilizopigwa utathibitisha nambari ya Dkt Ruto imo ndani ya ushahidi uliokusanywa wakati wa upelelezi, kinyume na pingamizi la Bw Gicheri kupitia kwa wakili wake.

Bw Steynberg aliongoza kesi hiyo tangu ilipoanza kwa niaba ya mkuu wa mashtaka, Bw Karim Khan, ambaye alijiondoa kwa vile alikuwa wakili mkuu wa Dkt Ruto wakati aliposhtakiwa ICC.

Hata hivyo, nakala iliyowasilishwa na upande wa mashtaka ilionekana kumwondolea lawama Bw Khan, ikionyesha njama za kuvuruga mashahidi zilifanywa bila mawakili wa naibu rais kujua.

Bw Gicheru kupitia kwa wakili Michael Karnavas, alitumia taarifa yake ya mwisho mahakamani kupuuzilia mbali ushahidi wote uliotolewa dhidi yake akidai ulikuwa kwa msingi wa uvumi, na kutegemea mashahidi wasioaminika.

Bw Karnavas alidai kuwa, mashahidi walioitwa waliwahi kutoa ushahidi wa uongo kwa hivyo madai yao hayastahili kutegemewa katika uamuzi utakaotolewa.

“Ukienda hotelini uagize supu ya nyama, uone yapendeza kwa macho, uonje kijiko kimoja uhisi ule tamu. Kisha ukila nyama kwanza na ya pili ni tamu na laini lakini ile ya tatu upate imeoza, utafanyaje? Utaendelea kuonja zote zilizobaki ili upate zilizo nzuri, ama utaamua kuachana nayo na uagize chakula kingine tofauti ama vyema zaidi, uondoke uende hoteli nyingine?” akauliza, akitaka ushahidi wote utupwe nje na mahakama iamue mteja wake hana hatia.

Jaji Miatta Maria Samba, alisema uamuzi utakaotolewa utazingatia sheria na ushahidi uliotolewa katika kesi hiyo pekee.

  • Tags

You can share this post!

Wajackoyah apata mpiga debe anayemfanana

‘Cohen alilazimika kumuoa Sarah ili asirudishwe kwao’

T L