Nambari za masuala ya dharura zazinduliwa Kiambu

Nambari za masuala ya dharura zazinduliwa Kiambu

NA LAWRENCE ONGARO

GAVANA mpya wa kaunti ya Kiambu, Kimani Wamatangi, anaendelea kuweka mikakati dhabiti ili kufanikisha mipango yake ya kazi.

Mnamo Jumatatu alizindua namba za simu za Hotline zitakazotumiwa na wafanyakazi pahali popote iwapo kutatokea jambo la dharura.

Kulingana na Wamatangi, anataka kufanya kazi yake kwa uwazi bila kuwa na fitina na uonevu miongoni mwa wafanyakazi hao.

“Mimi kama gavana wenu nitakuwa mtumishi ambapo niko tayari kusikiliza maswala yote yanayoambatana na kazi niliyopewa kutekeleza. Kwa hivyo kila mfanyakazi afanye kazi bila kuwa na hofu yoyote ya kudhulumiwa na yeyote,” gavana alifafanua katika maelezo yake.

Namba maalum alizozindua rasmi kwa wafanyakazi za kutumia kwa jambo la dharura ni Safaricom Р0742 000 888. Halafu ya Airtel ni  0103 000 888.

Alisema iwapo namba hizo zitatumiwa kwa njia inayostahili bila shaka kutakuwa na mwelekeo wa mambo kwa njia ifaayo.

“Ninajua ndiyo tumeanza mwendo ambapo tukishirikiana pamoja bila shaka kaunti ya Kiambu itakuwa kielelezo kwa kaunti nyingine za hapa nchini,” alifafanua katika maelezo yake.

Kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa, gavana huyo amezuru kaunti yote ya Kiambu na kufanya mikutano tofauti na wafanyakazi wote kwa lengo la kuelewa jinsi walivyokuwa wakiendesha shughuli zao za kazi katika serikali iliyopita.

Katika mkutano na wafanyakazi hivi majuzi kutoka Thika, Ruiru, Gatundu, na Juja, alieleza jinsi mipango yake ya baadaye inavyostahili kuendeshwa.

Alisisitiza sana umuhimu wa kukusanya fedha za kuegesha magari na za maeneo ya matimbo ya mawe.

Alisema yeyote atakayezembea katika sekta hiyo atapigwa kalamu bila kusita.

Aliwaagiza wakuu katika sekta tofauti wahesabu wafanyakazi wote na kuwasilisha majina kamili mbele yake.

Jambo lingine akasisitiza umuhimu wa mfanyakazi kuweka saini jina lake kila mara anaporipoti kazini na wakati anapotoka jioni.

Alisema ukosefu wa mishahara kwa miezi kadha kwa wafanyi kazi ni swala litakaloshughulikiwa haraka iwezekanavyo, ili kila mfanyakazi awe na motisha ya kufanya kazi kwa bidii.

  • Tags

You can share this post!

Mhariri wa KBC Millicent Owuor kujua hatima yake Oktoba 11

TAHARIRI: Serikali ikabili ufisadi iwapo inataka ustawi

T L