Kimataifa

NAMIBIA: Jamii inayokaribisha wageni kwa ngono

December 14th, 2018 2 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

HESHIMA na ukaribisho unaofaa ni desturi ya jamii za Afrika pale zinapopata mgeni. Ni jambo la wazi kuwa nyimbo, mashairi, hadithi na vyakula ni baadhi tu ya mambo ambayo Waafrika na Wakenya haswa humkaribisha mgeni nayo, ili ajihisi kupendwa.

Hata hivyo, jamii moja kutoka Namibia hutumia mbinu ya aina yake kufanyia makaribisho wageni wake, na ambayo inaonekana kukinzana na imani na desturi za jamii nyingi za barani.

Watu wa makabila ya Ovahimba na Ovazimba ambao wanaishi maeneo ya Kunene na Omusati, Kaskazini mwa Namibia wamedumisha desturi ya kuwakaribisha wageni wake kwa ngono, jambo ambalo hata licha ya mkoloni kuja na kubadili mambo mengi limesalia sehemu ya jamii hiyo.

Makabila hayo yana takriban watu 50,000, huku yakiishi kwa utamaduni wa kitambo wa wanawake kulea watoto na kulinda mifugo, nao wanaume kushiriki uwindaji.

Lakini utamaduni wao ambao ni wa kushangaza ni ule wa mgeni kukaribishwa kwa ngono pale anapotembelea familia fulani, tena kwa kulala na mume wa boma alilotembea (ikiwa ni mwanamke) ama mke wa boma hilo (ikiwa ni mwanaume).

Anapofika mgeni mwanaume, mzee mwenye boma ataonyesha kumkaribisha kwa kumruhusu kulala na mkewe usiku katika kitanda chao cha ndoa, ambapo mgeni na mkewe huyo wana uhuru wa kufanya mapenzi bila kuulizwa na yeyote.

Aina hiyo ya ukaribisho inafahamika kama “Okujepisa Omukazendu” baina ya jamii hiyo.

Mwanaume mwenye boma atalala katika chumba kingine, ama ikiwa hakipo alale nje.

Kulingana na jamii hiyo, desturi hiyo imefaa ndoa zake kwani wanandoa hawana wivu. Mwanamke hana usemi kwani ni mumewe anayeamua, japo anaweza kukataa kufanya ngono na mgeni, lakini watalala kitanda kimoja.

Bilashaka ni utamaduni ambao unaweza kumfanya yeyote kuzuru eneo wanapoishi jamii hiyo Namibia, kutokana na upekee wa desturi hiyo.

Mbali na itikadi hiyo waliyodumisha miaka na mikaka, watu wa makabila hayo aidha hushiriki ndoa za wake wengi, huku baba akiamua mwanaume atakayemwoza bintiye kwake, pale anapohitimu umri.

Wanawake wa jamii hiyo aidha badala ya kuoga hujingarisha mili kwa kutumia moshi na kusugua mwili kisha kujipaka manukato, aina ya kuoga ambayo mababu na mababu walitumia.