Michezo

Namibia yazima Senegal raga ya chipukizi ikianza jijini Nairobi

April 4th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA watetezi Namibia wameanza mashindano ya Bara Afrika ya raga ya wachezaji 15 kila upande ya Barthes Trophy ambayo ni ya kufuzu kushiriki Junior World Rugby Trophy (JWRT) kwa kishindo baada ya kupepeta Senegal kwa alama 45-12 jijini Nairobi, Alhamisi.

Namibia iliongoza pembamba 19-7 wakati wa mapumziko uwanjani KCB Sports Club mtaani Ruaraka kabla ya kuzidia Senegal maarifa kabisa katika kipindi cha pili.

Ushindi huu unaweka Namibia katika fainali itakayosakatwa Aprili 7. Nayo Senegal imeteremka hadi mechi ya kutafuta mshindi wa medali ya shaba, ambayo itatanguliwa kusakatwa kabla ya fainali.

Mshindi kati ya wenyeji Kenya almaarufu Chipu na Tunisia baadaye Alhamisi atajikatika tiketi ya kumenyana na Namibia katika fainali.

Timu itakayoibuka bingwa wa Afrika itaingia mashindano ya dunia ya JWRT yatakayofanyika nchini Brazil hapo Julai 9-21 mwaka 2019.

Chipu ilipigwa na Namibia katika fainali za mwaka 2013, 2014, 2016 na 2017 na 2018 na inatumai itapata ufunguo wa kunyakua tiketi moja ilioko mezani.

Hata hivyo, kabla ya kujikatia tiketi ya fainali, Kenya lazima ichape Tunisia.

Timu itakayopoteza mchuano huu itakabana koo na Senegal kuamua nani anasalia katika mashindano haya ya daraja ya juu kabisa ya chipukizi. Shoka litaangukia timu itakayovuta mkia.