Makala

Safari ya helikopta 16 na magari 150 ya kivita kutoka Amerika hadi Kenya

May 26th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

KATIKA ziara ya Rais William Ruto nchini Amerika ambayo ilitamatika Ijumaa, mwenyeji wake, Rais Joe Biden alitangaza kwamba ushirika wao umezaa matunda kemkem miongoni mwayo ikiwa ni Kenya kupata ndege 16 za usalama pamoja na magari 150 ya doria spesheli.

Ndege hizo aina ya helikopta, ilitangazwa kwamba zitawasili nchini kati ya Agosti 2024 na Januari 2025.

Aidha, magari hayo ya doria ambayo risasi haiwezi ikapenya, yalitambuliwa kama aina ya M1117.

Nazo ndege hizo aina ya helikopta zimetambuliwa kama muundo wa Huey na MD-500s, zikiwa ni nane kwa kila aina.

Swali ambalo linasumbua wengi ni jinsi shehena hiyo itakavyotua nchini Kenya ikizingatiwa kwamba sio mzigo wa kufungwa kwa gunia na kisha kukabidhiwa bebabeba au bodaboda afikishe kunakostahili.

Kwa mujibu wa Bw James Makau, ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uchukuzi wa kimataifa, vifaa hivyo vinaweza tu vikafika nchini Kenya kupitia ama ndege angani au baharini kwa kutumia meli.

“Kuna ndege kubwa za kubeba mizigo hasa ndege aina ya A400M na C-130 ambazo zinaweza zikawasilisha helikopta hizo. Lakini kwa kuwa hizi ambazo Amerika imeituza Kenya ni nyingi, naona tu zikiwasili nchini kupitia meli,” akasema Bw Makau.

Alisema muda ambao umetolewa wa kuwasilisha vifaa hivyo hapa nchini unaonyesha wazi kwamba huenda meli itumike.

“Kutoka Amerika hadi hapa nchini Kenya kupitia uchukuzi wa meli, shehena huchukua kati ya siku 60 na 75. Ukiangalia tarehe ambazo zimepeanwa za kupokezwa ndege hizo, utapata zinawiana na uchukuzi wa meli,” akasema Bw Makau.

Alisema meli iko na uwezo wa kubeba helikopta 20 kwa mpigo.

Lakini pia helikopta na ndege nyingine zinaweza kupaa kutoka nchi mtengenezaji au muuzaji na mtoaji hadi kwa nchi mnufaika au mnunuaji na zinaweza kuenda kujaza mafuta njiani katika mataifa rafiki.

Kuhusu magari hayo ya kivita, alisema kwamba kuna ndege kubwa ambayo pia inaweza ikayabeba kwa mpigo mmoja.

“Hizo ndege kubwa za uchukuzi zinaweza zikabeba magari 80 Kwa wakati mmoja. Pia, meli inaweza ikayaleta nchini Kenya. Uamuzi utakuwa wa mataifa hayo mawili kwa mujibu wa mkataba ulioko,” akasema Bw Makau.

Rais Ruto alitangaza kwamba kuwasili kwa vifaa hivyo vya kivita kutaimarisha juhudi za nchi kujiweka imara kiusalama ikikabiliana na changamoto zilizoko hasa za ugaidi na ujangili.

Mara si moja, Kenya imelazimika kuvizia wapiganaji wa Al-Shabaab ambao hulenga na kutekeleza mashambulio nchini.