Makala

Namna wazee walivyoathirika na janga la corona

September 12th, 2020 2 min read

Na WINNIE ATIENO

KWA miaka na mikaka, watawa wanaoshughulikia wazee katika nyumba ya wakongwe huko Mombasa walikuwa wanatanga na njia sehemu kadhaa wakiomba misaada.

Lakini maisha yalibadilika pindi Kenya iliponakili visa vya corona; hali iliyosababisha serikali kulifunga jiji la Mombasa ili kupunguza kuenea kwa virusi hivyo.

Jiji hilo lilikuwa na visa vingi vya maambukizi na liliongoza kwa watu walioaga dunia kutokana na Covid-19.

Hali hiyo ililemaza shughuli katika Nyumba ya Wazee mtaani Tudor ambao wanategemea misaada kwa wafadhili na wahisani kila wakati watawa walikuwa wakienda kuomba omba katika maduka makubwa, bandarini Mombasa na hata soko kubwa la Kongowea.

“Tulikuwa tunaenda kuomba msaada wa wahisani mitaani lakini tangu jiji la Mombasa kufungwa tuliachwa katika njia panda. Tulikuwa hatuwezi tena kwenda kuomba misaada kwa sababu hawa wazee walitajwa kuwa kwenye hatari ya maambukizi kwa hivyo hatungeweza kuhatarisha maisha yao. Hivi tunaendelea kutaabika na kupitia hali ngumu. Tunawaomba wahisani wajitokeze na wale wamekuwa wakitusaidia tunawaombea mema,” akasema Mtawa Grace Kinyua wakati wakuu wa kampuni ya Hazina Sacco walienda kuwapa misaada ya dawa, sanitaiza na mahitaji mengine muhimu.

Maafisa wa Hazina Sacco wakiwa na watawa wanaowatunza wazee katika kituo cha wakongwe eneo la Tudor. Picha/ Winnie Atieno

Wakati huo, Mkurugenzi wa Hazina Sacco Bw Dickson Okungu aliwasihi Wakenya kusaidia wanyonge katika jamii.

“Kama shirika tutaendelea kusaidia wale walioathirika na janga la corona. Wakenya tunafaa kwua katika mstari wa mbele kusaidia wenzetu walioathirika,” alisihi.

Wazee hao ambao wanategemea dawa za kisukari, presha na saratani walipata afueni baada ya Bw Okungu walipoenda kutoa misaada hiyo.

“Wanafaa dawa hizi ili waimarishe afya zao. Wanameza dawa kila siku. Tunawasihi wakenya wengine wajitokeze na kutusaidia. Tunapitia changamoto kadha wa kadha, hususan bili yetu ya stima, mwaka jana kampuni ya Umeme ilitukatia stima tukataabika kwa wiki moja,” alilia Bi Kinyua.

Hata hivyo wameanza mikakati ya kuweka sola ili kupunguza ghamara ya umeme.

Alitaja changamoto zingine ikiwemo kuvuja kwa dari wakati kunanyesha na majitaka kuingia ovyo. Mtawa huyo alisema nyumba hiyo ya wazee ambayo ina miaka 51 inafaa kufanyiwa ukarabati kwani imezeeka.

Watawa hao wamekuwa wakiwashughulikia wazee hao ambao wengine wametelekezwa na familia zao.

Katika nyumba hiyo, wamekuwa wakipata upendo, mavazi, chakula na hata matibabu wanapougua.

Wale wanaaga dunia huzikwa katika eneo la Mbaraki.