Afya na Jamii

Namna ya kujikinga dhidi ya miale hatari ya jua

February 21st, 2024 2 min read

NA LABAAN SHABAAN

JUA kali limekuwa likishuhudiwa sehemu tofauti nchini kiasi cha kufanya watu kuogopa kutoka nje ila wanalazimika tu sababu ya kutafuta riziki.

Wanaoishi katika nyumba za mabati kotekote wanapitia kipindi kigumu utabiri ukionyesha joto litapanda hadi nyuzijoto 39 juma hili.

Idara ya utabiri wa hali ya hewa imewaambia Wakenya kuwa hali itaendelea hivyo juma hili katika maeneo yafuatayo: Nairobi, Embu, Meru, Kiambu na Muranga zitakuwa na joto kiasi cha nyuzi joto 38.

Sehemu ambazo zimezoea kiangazi kama vile Turkana na Samburu zitazidiwa na joto hadi nyuzi joto 39.

Utabiri wa hali ya hewa uliotolewa na Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo (IGAD) inaonyesha mashariki ya Kenya itapokea makali ya juu ya jua katia ya Machi na Mei.

Ila, huu si wakati ambapo nchi hushuhudia msimu wa mvua nyingi?

Miaka ya hivi karibuni, mabadiliko ya hali ya anga yameathiri sana misimu iliyozoeleka.

Wakenya wafanye vipi kustahimili joto?

Mwanasayansi wa hali ya hewa na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi, Dkt Cromwel Lukorito anashauri wananchi wahakikishe wanakunywa maji ya kutosha kutunza afya.

Kadhalika wito umetolewa kwa Wakenya kubeba miavuli ya kuweka mikobani tayari kuichomoa kujikinga na jua kali pamoja na kuvaa mavazi mepesi.

Njia nyingine ya kujilinda ni kutafuta kivuli na kama ni lazima ufanye kazi juani unashauriwa kuvaa kofia na nguo nyepesi inayofunika mikono na miguu.

Kipindi cha jua kali si cha kufanya kazi bila kupumzika.

Ili kuimarisha afya, mfanyakazi anatakiwa kujitathmini na kupumzika kama inavyohitajika.

Shirika la Bima la Liaison Group limetaja kuwa Watoto wako katika hatari kubwa ya kuathiriwa na jua kali.

Walezi na wazazi wanaelekezwa kufuata tahadhari zilizotolewa ili kulinda watoto ambao hupenda kucheza nje kwenye jua kali.

Miale ya jua kupitiliza huwa hatari kwa afya

Mionzi mikali ya jua inaweza kuharibu mishipa inayoshikanisha tishu za mwili.

Isitoshe, pia kuharibu vitamini A katika ngozi na kuongeza hatari ya kupata saratani ya ngozi.

Vile vile, jua lenye joto la juu husababisha ugonjwa wa macho (cataracts) na kuzidisha makali ya maradhi yanayosababishwa na virusi.

Miale ya jua husaidia mwili kuzalisha vitamin D lakini inaweza kuleta hatari ya kansa.

Kwa hivyo kupata kiwango sahihi ya mwanga wa jua ni muhimu sana.