Namwamba aahidi kufufua sekta ya michezo nchini

Namwamba aahidi kufufua sekta ya michezo nchini

NA JOHN ASHIHUNDU

WAZIRI mpya wa Michezo, Ababu Namwamba ameahidi kufufua sekta ya spoti kote nchini mara tu atakapoanza kutekeleza wajibu wake rasmi.

Mbunge huyo wa zamani wa eneobunge la Budalang’i ni miongoni mwa watu walioteuliwa kwenye Baraza la Mawaziri katika Serikali mpya ya Rais William Ruto mapema juma hili.

Wakenya wengi wameonyesha matumaini yao kwa Namwamba ambaye anafahamu zaidi maswala ya Michezo, ikikumbukwa kwamba alikuwa katika kamati kuu ya uongozi wa klabu ya AFC Leopards alipokuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu, kabla ya kuwa Naibu Waziri wa Michezo wakati wa Serikali ya Nusu-Mkate.

Alipokuwa usukani, Namwamba anakumbukwa kwa kusukuma Serikali kuweka Sheria ya Michezo ya 2013, iliyolenga kufufua shughuli za michezo kuanzia mashinani.

“Sasa ni miaka tisa tangu wakati huo, na iwapo Bunge litanikubalia niendeshe Wizara hii kwa mara nyingine, nitakamilisha malengo yangu. Namshukuru rais Ruto kwa kunitambua na kunipa jukumu hili,” Namwamba ambaye amekuwa Waziri Msaidizi katika Wizara ya Maswala ya Kigeni aliongeza baada ya kupewa jukumu jipya Jumanne, wiki hii.

Namwamba atachukuwa mamlaka kutoka kwa Amina Mohamed aliyehudumu kama Waziri wa Michezo tangu Machi 2019.

Hata hivyo, Ababu anakabiliwa na changamoto kutokana na vita kati ya Serikali na Fifa, wakati huu Kenya imepigwa marufuku na Shirikisho hilo la Kimataifa la Soka.

Mara tu baada ya kuteuliwa kama Waziri wa Michezo, Namwamba alisema kuna haja ya Serikali kuzungmza na Fifa kuondoa mvutano huo ili Kenya ikubaliwe tena kushiriki katika mashindano ya kimataifa.

Baada ya marufuku hiyo ya tangu Februari 25, 2022, Hrambee Stars imezimwa kushiriki katika mechi za Mataifa ya Afrika (Afcon) za kufuzu kwa fainali za 2023.

Marufuku hiyo ilitokea baada ya Serikali kupiga marufuku kama ya Nick Mwendwa na kuteua kamati ya mpito kusimamia maswala ya kandanda nchini.

Wakati huo huo, msimamizi maarufu wa michezo, Twaha Mbarak ni miongoni mwa watu mashuhuri waliompongeza Rais Ruto kwa kumteua Namwamba kwa Waziri wa Michezo.

Mbarak alimtaja Namwamba kama mtu muaminifu anayeheshimu sharia, mbali na kuwa na ufahamu mkubwa kuhusu maswala ya michezo.

Alisema anaamini Namwamba ndiye mtu atakayesuluhisha vuta nikuvute kati ya Serikali na Fifa.

  • Tags

You can share this post!

Naibu chifu ajivunia usalama katika kaunti ndogo ya Chonyi...

Fuliza: Ruto sasa aokoa mahasla riba ikipungua

T L