Michezo

Nandwa pazuri kubwaga Shikanda, Odipo na kuwa kocha mpya wa Nzoia Sugar

November 18th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA wa zamani wa Harambee Stars, James Nandwa, yuko pazuri zaidi kupokezwa mikoba ya Nzoia Sugar ambao wamekuwa bila mkufunzi tangu Machi 2020 baada ya Collins ‘Korea’ Omondi kutimuliwa kwa sababu ya matokeo duni.

Chini ya Korea, Nzoia Sugar waliambulia nafasi ya 15 kwa alama 13 kwenye msimamo wa jedwali la vikosi 18 vya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) mnamo 2019-20.

Kwa mujibu wa mwenyekiti Evance Kadenge, klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) ilikamilisha mchakato wa kuwahoji baadhi ya wakufunzi waliotuma maombi ya kazi kambini mwao mnamo Jumanne katika afisi za kampuni ya sukari ya Nzoia Sugar, Bungoma.

Mbali na Nandwa ambaye pia amewahi kuwa mkufunzi mkuu wa Thika United, wengine waliohojiwa ni kocha wa zamani wa SoNy Sugar Leonard Odipo, John Nams, Ibrahim Shikanda na Sylvester Mulukurwa ambaye kwa sasa anasaidiana na kocha wa makipa John Muraya kushikilia mikoba ya Nzoia Sugar.

Odipo amewahi kudhibiti mikoba ya Nairobi Stima inayoshiriki Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL) naye Shikanda amewahi kuwa kocha msaidizi wa Bandari FC kisha Azam FC nchini Tanzania.

Nzoia walianza shughuli ya kutafuta kocha mpya mnamo Oktoba na wadhifa huo ulivutia jumla ya wakufunzi 24 akiwemo kocha wa zamani wa Shabana FC, Gilbert Selebwa, aliyekuwa kocha msaidizi wa KCB Ezekiel Akwana, John Kamau, Francis Xavier, George Maina na Yusuf Chipo miongoni mwa wengine.

Kamau ameteuliwa kuwa msaidizi wa aliyekuwa kocha wa Harambee Stars, Francis Kimanzi, katika kikosi cha Wazito FC kilichomtimua majuzi Fred Ambani na benchi yake nzima ya kiufundi iliyomjumuisha pia kocha Salim Babu ambaye sasa ameajiriwa na Kisumu All Stars.

“Tumesalia na wawaniaji watatu wakuu kwa sasa – Nandwa, Odipo na Shikanda. Tunatazamia Idara ya Uajiri kutangaza kocha mpya wa Nzoia Sugar kufikia mwisho wa wiki hii kabla ya kikosi kuanza maandalizi kwa minajili ya msimu mpya,” akasema Kadenge.

Kikosi hicho kilichopokezwa basi jipya laviti 51 na Sh2 milioni kutoka kwa Rais Uhuru Kenyatta majuzi, kilijisuka upya kwa kusajili wanasoka 12 baada ya kuagana na wachezaji tisa muhula huu.

Mbali na Daniel Kakai aliyetokea AFC Leopards kwa mkopo, masogora wengine waliosajiliwa na Nzoia Sugar ni Gabriel Wandera (Tusker) na Elivis Ronack Otieno (Gor Mahia).

Mustapha Oduor, Moses Mudavadi na Cliff Kasuti (wote Bandari FC), Felix Oluoch (Posta Rangers), kiungo Eric Mango (KCB) na Titus Kapchanga (St Anthony’s Kitale), Kevin Maliachi (APS Bomet) inayoshiriki Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL), Brian Wanyonyi na Jeremiah Juma.

Mohammed Nigol, Robert Abonga, Chris Wesamba, Masoud Juma, Abraham Kipkosgei, Faraj Kibali, Boris Kwezi, Jeremiah Wanjala na Vincent Odongo aliyeyoyomea Kariobangi Sharks ni miongoni mwa wachezaji ambao walikatiza uhusiano na Nzoia Sugar muhula huu.

“Lengo letu ni kusalia na idadi ya wachezaji ambao tunaweza kumudu mahitaji yao kifedha,” akaongeza Kadenge kwa kufichua kwamba wamekuwa wakitafuta kocha ambaye ana leseni ya daraja la C kutoka kwa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF).

Kadenge aliyepokezwa uenyekiti wa Nzoia mnamo Februari 2020 baada ya kuondoka kwa Yappets Mokua.