Habari

Nani anataka kumuua Ruto?

June 25th, 2019 2 min read

Na PETER MBURU

UCHAFU umeingia siasa za kumrithi Rais Uhuru Kenyatta 2022, kufuatia kuchipuka kwa madai kuwa kuna njama ya kumzima Naibu Rais William Ruto kwa kumuua.

Jumatatu mawaziri watatu kutoka eneo la Mlima Kenya walifika katika makao makuu ya Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) kurekodi taarifa kuhusu madai ya kushiriki mpango huo wa kumwangamiza Dkt Ruto.

Hata hivyo, mawaziri Peter Munya (Biashara), Sicily Kariuki (Afya) na Joe Mucheru (Habari na Teknolojia) walipuzilia mbali madai hayo kama yasiyo na msingi.

Habari hizo ziliibuka huku barua inayodaiwa kuandikwa kwa Rais Kenyatta na waziri mwingine, ambaye anapinga njama hiyo ya mauaji, ikisambaa mitandaoni.

‘Waziri’ huyo amelalamika kuhusu mikutano ambayo mawaziri fulani kutoka Mlima Kenya wamekuwa wakiandaa, ajenda mojawapo ikiwa kumuangamiza Naibu Rais.

Barua hiyo, hata hivyo, haionyeshi waziri aliyeiandika kwani imefutwa sehemu kadhaa. Lakini amewataja mawaziri wengine wanaohudhuria mikutano hiyo kuwa Bw Munya, Bi Kariuki, Bw Mucheru na James Macharia (Uchukuzi).

Anasema mikutano hiyo pia hushirikisha makatibu wa wizara na wakuu wa mashirika ya kiserikali kutoka Mlima Kenya.

Mawaziri Mwangi Kiunjuri (Kilimo) na Margaret Kobia (Utumishi wa Umma) hawajatajwa kwenye barua hiyo kama miongoni mwa wanaohudhuria mikutano hiyo.

Barua hiyo inasema kuwa mkutano huo uliitishwa na Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Karanja Kibicho, na moja ya ajenda ilikuwa ni kujadili mbinu za kumzima Dkt Ruto ukiwemo uwezekano wa kumuua.

“Katibu (Kibicho) alieleza mkutano kuwa lazima Naibu Rais azimwe. Lakini kilichonitia wasiwasi zaidi ni hatua yake kurejelea ajali ya helikopta iliyoua Prof George Saitoti mnamo 2012. Alisema kuwa hata Saitoti, ambaye alikuwa anataka kuwania urais, alizimwa. Kwani huyu anafikiria yeye ni nani?” inasema.

Kwenye barua hiyo, ‘waziri’ anayedaiwa kuiandika anaomba akubaliwe kutohudhuria mikutano hiyo kwani katika maisha yake hajawahi kuhusika katika siasa wala kupanga mauaji.

Wakizungumza na wanahabari jana baada ya kukutana na maafisa wa DCI, mawaziri hao walisema walifika huko baada ya Dkt Ruto kupigia simu DCI, akisema walikuwa wakipanga kumuua.

“Wametuthibitishia kuwa Naibu Rais alipiga simu na akalalamika kuwa kuna mawaziri na maafisa wakuu serikalini ambao wamekuwa wakikutana katika mkahawa mmoja Nairobi kupanga kumuua,” akasema Bw Munya.

Kutorekodi taarifa

Hata hivyo, walisema mbali na kupiga ripoti, Naibu Rais hakuwa amerekodi taarifa yoyote kwa polisi, na hivyo hawangeweza kujibu madai yake.

“Naibu Rais hajarekodi taarifa yoyote kuhusu malalamishi yake. Tumewataka maafisa waliopigiwa simu kuandika kile walichoambiwa naye ili tuweze kujibu. Ikiwa wangeandika walichoambiwa, tulikuwa tayari kurekodi taarifa zetu,” Bw Munya akasema.

Pia walisema maafisa wa DCI hawakuthibitisha uhalali wa barua ambayo inadaiwa kuandikwa na mmoja wa mawaziri.

Lakini Bw Munya alithibitisha kuwa mawaziri, makatibu wa wizara na maafisa wengine wakuu serikalini kutoka Mlima Kenya, wamekuwa wakikutana katika mkahawa wa La Mada kwenye barabara ya Thika Road kujadili masuala ya maendeleo ya eneo hilo.

“Hakuna wakati tumewahi kukutana mahali popote kupanga kumuua Naibu Rais ama mtu yeyote mwingine. Tumekuwa tukikutana La Mada na tutaendelea kukutana kuhusu changamoto zinazokumba eneo la Mlima Kenya,” Bw Munya akasema.

Alieleza kuwa waliagizwa na Rais Kenyatta wawe wakifanya mikutano hiyo baada ya wabunge kutoka Mlima Kenya kulalamika kuwa miradi ya maendeleo ilikuwa imekwama.