Michezo

Nani ataibwaga KCB kwenye Ligi Kuu ya Raga?

February 26th, 2018 1 min read

Mchezaji wa timu ya Impala Micheal Mugo (kushoto) akabiliana na Nesta Oketch wa KCB katika mechi ya awali. Picha/ Maktaba

Na GEOFFREY ANENE

KLABU ya KCB imedumisha rekodi ya kutoshindwa na Kabras Sugar kwenye Ligi Kuu ya Raga ya Kenya hadi mechi saba baada ya kuibwaga 41-12 uwanjani Ruaraka jijini Nairobi, Jumamosi.

Viongozi KCB, ambao wanajivunia kulemea Kabras mara sita na kupata sare moja tangu Kabras waingie Ligi Kuu mwaka 2014, wamezoa ushindi huo mkubwa kupitia wachezaji Darwin Mukidza, Peter Karia, Nick Ongeri, Brian Nyikuli na Felix Ojow.

Nyota Mukidza aliweka mabingwa watetezi KCB alama 3-0 juu kupitia penalti kabla ya Karia kupachika mguso ulioimarisha uongozi huo hadi 8-0.

Mukidza aliongeza mkwaju uliofanya KCB kufungua mwanya hadi 10-0.

Kabras ilijaribu kushambulia ngome ya KCB, lakini ikajipata chini 17-0 baada ya Ongeri kufunga mguso ambao Mukidza aliongeza mkwaju wake.

Mambo yaliharibikia KCB hata zaidi baada ya Nyikuli kuongeza mguso ambao pia uliandamana na mkwaju kutoka kwa Mukidza.

Penalti ya Mukidza mwanzo wa kipindi cha pili ilishuhudia KCB ikiongoza 27-0 kabla ya Kabras kupunguza mwanya huo hadi alama 20 baada ya kufunga mguso kupitia Mganda Philip Wokorach, ambaye pia alipachika mkwaju.

Ojow alifungia KCB mguso wa tano ulioweka wanabenki wa KCB mbele 32-7. Mukidza aliongeza mkwaju wa mguso huo.

Dakika chache baadaye, Ojow alionyeshwa kadi ya njano na kuwezesha Kabras kutumia nguvu ya kuwa na mchezaji mmoja zaidi uwanjani kufunga mguso bila mkwaju. Mukidza aligonga msumari wa mwisho baada ya kupata mguso na mkwaju.

Ushindi huu umetosha kuipa KCB tiketi ya kuandaa mechi moja ya nusu-fainali. KCB imefuzu moja kwa moja kushiriki nusu-fainali ikiwa imesalia na mechi moja kumaliza msimu wa kawaida wa ligi hii ya klabu 12.

Matokeo (Februari 24, 2018):

Kenya Harlequins 43-17 Kisii

KCB 41-12 Kabras Sugar

Mwamba 34-20 Blak Blad

Homeboyz 123-11 Mombasa

Nakuru 24-11 Nondescripts

Impala Saracens 23-10 Strathmore Leos