Nani atapaa Kiambaa?

Nani atapaa Kiambaa?

BENSON MATHEKA na SIMON CIURI

UCHAGUZI mdogo wa kiti cha eneobunge la Kiambaa unaofanyika leo, unaanika wazi ushindani mkali kati ya viongozi wawili wa Jubilee waliokuwa marafiki wakubwa wa kisiasa kabla ya kugeuka kuwa mahasimu wakuu, Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto.

Kwenye uchaguzi huo, Dkt Ruto anaunga mgombeaji wa chama cha United Democratic Alliance (UDA), John Njuguna, dhidi ya Bw Kariri Njama wa chama tawala cha Jubilee ambaye anaungwa na Rais Kenyatta.

Uchaguzi huo unaonyesha jinsi ambavyo uhusiano kati ya viongozi hao wawili umedorora tangu walipochaguliwa kwa muhula wa pili 2017. Hii ni tofauti na muhula wa kwanza wa Jubilee kati ya 2013 na 2017 ambapo walishirikiana kwa karibu katika utawala na kuvumisha Jubilee.

Dkt Ruto aliyetengwa serikalini kwa kupinga handisheki kati ya Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, amekuwa akiendeleza kampeni dhidi ya mkubwa wake na wachanganuzi wa siasa wanasema kwamba ushindi wa mgombeaji wa UDA katika uchaguzi mdogo wa Kiambaa utakuwa ushindi dhidi Rais Kenyatta nao ushindi wa mgombeaji wa Jubilee utakuwa ushindi dhidi ya Dkt Ruto.

Kulingana na wakili Kibe Mungai, kushindwa kwa Jubilee katika kaunti ya nyumbani ya Rais Kenyatta kwa mara ya pili kunaweza kuathiri siasa za urithi 2022.

“Kushindwa kwa Jubilee katika kitovu cha ngome yake ya siasa kutakuwa pigo kwa kuwa ujumbe ambao matokeo hayo yatawasilisha utakuwa umaarufu wake (Rais Kenyatta) unapungua na utakuwa na athari za siasa za urithi mwaka wa 2022,” Bw Mungai asema.

Mwezi mmoja uliopita, Jubilee ilishindwa kwenye uchaguzi mdogo wa eneobunge la Juja ambalo pia liko Kaunti ya Kiambu, mwaniaji wa chama cha Peoples Empowerment Party (PEP) George Koimburi kinachohusishwa na mshirika wa Dkt Ruto, alipombwaga Susan Waititu Wakapee wa chama tawala.

Bw Mungai anasema ushindi wa mgombeaji wa chama cha Dkt Ruto kwenye uchaguzi wa Kiambaa utadhihirisha kuwa kampeni yake ya Hasla imepata nguvu.

Rais Kenyatta ambaye amekuwa akimkosoa Dkt Ruto hadharani kiasi cha kuashiria kuwa hatamuunga mkono 2022, anataka kutumia uchaguzi mdogo wa leo Kiambaa kuthibitisha angali maarufu katika ngome yake ya siasa ya Mlima Kenya.

“Msiruhusu mtu kumuaibisha Rais Kenyatta katika ngome yake,” mbunge wa Kieni Kanini Kega aliwaambia wapigakura wa Kiambaa kwenye kampeni za mgombeaji wa Jubilee Kariri Njama.

Rais Kenyatta aliwatuma wabunge wa Jubilee Mlima Kenya kumpigia debe Bw Njama huku washirika wa Dkt Ruto eneo hilo wakiongoza kampeni za Bw Njuguna.

Kariri Njama wa Jubilee. Picha/ Maktaba

Kulingana na mdadisi wa siasa Mark Bichachi, uchaguzi mdogo wa Kiambaa ni vita vya ubabe kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto.

“Uamuzi wa watu wa Kiambaa utakuwa wa kuunga au kukataa Rais Kenyatta. Ni uchaguzi muhimu si kwa watu wa Kiambaa tu bbali kwa Rais Kenyatta pia,” asema.

Alhamisi wiki jana, Rais Kenyatta alikutana na Bw Njama katika Ikulu ya Nairobi.

Bw Bichachi aanasema iwapo mgombeaji wa UDA, atashinda, Dkt Ruto atakuwa na nguvu za kudai ni maarufu eneo la Mlima Kenya kuliko Rais Kenyatta.

Kampeni za Jubilee katika eneobunge hilo ziliongozwa na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Taifa, Bw Amos Kimunya, Mbunge wa Cherangany, Joshua Kutuny ambaye ni naibu katibu mkuu wa chama tawala, mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Wambugu, Kanini Kega wa Kieni na Peter Mwath, Jude Njomo (Kiambu Mjini ) na Gichuki Mugambi (Othaya) kati ya wengine huku Rais Kenyatta akizifuatilia kwa karibu.

Kulingana na mbunge wa Mathira Bw Rigathi Gachagua ambaye pamoja na Kimani Ichung’wah (Kikuyu), Ndindi Nyoro (Kiharu), Alice Wahome (Kandara), Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata na Seneta wa kuteuliwa Millicent Omanga waliongoza kampeni za UDA, ushindi wa Bw Njuguna utaonyesha chama kilicho na nguvu eneo la Mlima Kenya.

You can share this post!

Aliyeuawa kinyama alituzwa na Rais 2016

Polisi wahoji kijana aliyekiri kuteka na kuua watoto 13