Habari

Nani atapewa kiti cha Naibu Gavana kaunti ya Kiambu?

February 13th, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

BAADA ya gavana wa tatu Dkt James Nyoro kuapishwa rasmi aiongoze Kaunti ya Kiambu wiki mbili zilizopita, sasa macho yote yanalenga uteuzi wa naibu wake.

Baadhi ya viongozi wengi kutoka eneo hilo wanashinikiza afanye jambo la busara na kumteua mwanamke kujaza nafasi hiyo ya naibu wa gavana.

Hata hivyo viongozi hao wanataka eneo la Kiambu Mashariki lizingatiwe sana hasa ikitiliwa maanani kuwa viti vingi vya uongozi waliovipata ni wa kutoka Kiambu Magharibi.

Baada ya Bw Ferdinand Waititu kushtakiwa kwa ufisadi wa Sh588 milioni, Seneti iliamua ya kwamba hafai kuwa kwenye afisi ya umma huku akiwa amejitetea akisema hana hatia.

Kiambu Mashariki inajumuisha maeneo ya Ruiru, Juja, Thika, na Gatundu.

Halafu Kiambu Magharibi inaelekea maeneo ya Limuru, Kikuyu, Kabete, na Kiambaa.

 

Picha ya maktaba ya Bi Gladys Chania ambaye huwa mstari wa mbele katika masuala ya kisiasa na kijamii. Picha/ Maktaba

Yapo madai kwamba Dkt Nyoro anatoka eneo la kaunti ndogo ya Kikuyu, huku viongozi wengi walioteuliwa nao wakitokea Kiambu Magharibi.

Baadhi ya viongozi wanawake ambao wanakimezea mate kiti cha naibu wa gavana ni Gladys Chania, Esther Gathogo, Anne Nyokabi, Aquilline Gathendu, na Esther Wanjiru.

Kwa upande wa wanaume kuna David Gakuyo, na John Mugwe ambao inadaiwa walikuwa mstari wa mbele na Dkt Nyoro kumfanyia kampeni Bw Ferdinand Waititu kuingia uongozini mwaka wa 2017.

Mwenyekiti wa wafanyabiashara mjini Thika, Bw Alfred Wanyoike anasema kiongozi yeyote anaweza kuteuliwa mradi tu awe na ari ya kuchapa kazi bila ubaguzi wowote.

“Sioni ni kwa nini viongozi wanazungumzia uteuzi huo lakini cha muhimu ni kuona ya kwamba kiongozi ameteuliwa na atatekeleza majukumu yake bila ubaguzi,” alisema Bw Wanyoike.

Hata hivyo inadaiwa eneo la Kiambu Mashariki lina viwanda vingi na wafanyabiashara wengi wanatoka eneo hilo.

Hata asilimia 80 ya ushuru hutoka katika eneo hilo.

Lakini Bw Wanyoike alisema huu sio wakati wa kuwa na tamaa ya uongozi lakini ni vyema waliopewa dhamana kuongoza wanafaa kutendea wananchi haki kwa kuwapa huduma.