Michezo

NANI JOGOO? Arsenal itaepuka balaa 'kichinjioni' Anfield?

August 24th, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL, Uingereza

ARSENAL ina kibarua kigumu itakapoalikwa na Liverpool ambayo haijapoteza mechi sita zilizopita dhidi ya wapinzani hawa uwanjani Anfield.

Pia, Arsenal ya kocha Unai Emery haina ushindi dhidi ya vijana wa Jurgen Klopp katika mechi nane zilizopita.

Emery alikiri majuzi kuwa “kama kuna timu ambayo Arsenal haipendi kukutana nayo kabisa ni Liverpool.”

Baadhi ya wachanganuzi wanasema usemi huo wake ni kilio cha mtu aliyejawa na matumaini anapozuru Anfield.

Hata hivyo, dakika 90 zitamweka Mhispania huyu katika hali nzuri ya kuelewa kwa kina uwezo ambao vijana wake wanao wa kutafuta ufanisi msimu huu.

Baada ya kumaliza Ligi Kuu nje ya maeneo ya kushiriki Klabu Bingwa Ulaya kwa misimu mitatu mfululizo, mashabiki wengi walitilia shaka uwezo wa Arsenal.

Hata hivyo, uwekezaji uliofanywa na mmiliki Stan Kroenke wa kununua wachezaji kadhaa muhimu kabla ya msimu 2019/2020 kuanza umepunguza shaka hiyo.

Makali yapo

Arsenal ilianza msimu kwa kuchapa Newcastle 1-0 na Burnley 2-1.

Emery sasa ana makali zaidi baada ya sajili mpya Nicolas Pepe kuungana na Pierre-Emerick Aubameyang na Alexandre Lacazette katika idara ya ushambuliaji.

Kiungo wa Real Madrid, Dani Ceballos, ambaye yuko Arsenal kwa mkopo, alionyesha ustadi mkubwa alipochota kona iliyofungwa na Lacazette na krosi iliyokamilisha vyema na Aubameyang katika ushindi dhidi ya Burnley.

David Luiz, ambaye alitua Arsenal kutoka Chelsea saa chache kabla ya kipindi kirefu cha uhamisho nchini Uingereza kufungwa Agosti 9, anaimarisha safu ya ulinzi ya waajiri wake wapya.