Nani kama Wakenya!

Nani kama Wakenya!

NA WANDERI KAMAU

WAKENYA wamedhihirisha sifa ya kipekee mwaka huu, kutokana na utulivu mkubwa ambao wameendelea kuonyesha, wanapongojea Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutangaza matokeo ya uchaguzi wa urais.

Vigogo wa kisiasa walioshindwa kwenye nyadhifa tofauti walizokuwa wakiwania pia wamedhihirisha mwelekeo wa kipekee, wengi wao wakitoa jumbe za kukubali matokeo hayo au kusema wataenda mahakamani kuwasilisha malalamishi yao baada ya mahakama kurejelea vikao.

Baadhi ya wanasiasa ambao wamekubali matokeo ya uchaguzi hadharani ni aliyekuwa gavana wa Pokot Magharibi, Prof John Lonyangapuo, wabunge wa zamani Kanini Kega (Kieni), Jeremiah Kioni (Ndaragwa), Amos Kimunya (Kipipiri), Nixon Korir (Lang’ata), George Theuri (Embakasi Magharibi), Moses Kuria (aliwania ugavana Kiambu), Chris Wamalwa (aliwania ugavana Trans Nzoia), Prof Sam Ongeri (aliwania ugavana Kisii) kati ya wengine.

Baadhi ya wale ambao wamesema wataelekea mahakamani ni magavana wa zamani James Nyoro (Kiambu), Lee Kinyanjui (Nakuru), Ndiritu Muriithi (Laikipia) na Evans Kidero (Homa Bay).

Ni hali ambayo imeifanya Kenya kusifiwa pakubwa na raia wa mataifa tofauti duniani kwenye mitandao ya kijamii, wengi wakikiri kwamba hali ingekuwa tofauti katika mataifa yao.

Tangu uchaguzi huo kufanyika mnamo Jumanne, majadiliano makuu kwenye mitandao hiyo yamekuwa kuhusu vile Wakenya wamefanikiwa kudumisha utulivu wa kipekee, hali ambayo ni kinyume na chaguzi kadhaa zilizopita.

Baadhi ya mataifa ambayo yameongoza kuwapongeza Wakenya ni Tanzania, Uganda, Zambia, Afrika Kusini, Zimbabwe, Nigeria kati ya mengine.

“Msije mkatofautiana Wakenya kwa msingi wa tofauti za uchaguzi. Mumkatae mtu yeyote ambaye atajaribu kuleta uchochezi wa aina yoyote ile. Daima mkumbuke kuwa Kenya ni kubwa kuliko watu wawili. Kumbukeni kuwa tunawategemea pakubwa kama watu wa eneo la Afrika Mashariki, maanake mna maarifa mengi. Mmefanikiwa pakubwa katika masuala muhimu kama biashara. Msitofautiane maanake nyinyi nyote ni watoto wa baba mmoja. Idumu Kenya. Idumu Afrika Mashariki!” akaeleza raia mmoja kutoka Tanzania kupitia kwa video inayosambaa mitandaoni.

Nchini Uganda, raia wengi walieleza kushangazwa na kiwango cha utulivu nchini, ikizingatiwa kuwa serikali haikuwa imefunga mitandao ya kijamii, kinyume na hali ambayo hutokea mara nyingi nchini humo kila uchaguzi mkuu unapokaribia.

“Kwa kweli Kenya ni mfano wa kuigwa kama nchi ya amani. Hili ni jambo la kipekee,” akasema Isaiah Ssali kupitia mtandao wa Twitter.

Katika miji mikuu kama Nairobi, Mombasa, Kisumu na Nakuru, Wakenya wengi walionekana kuendelea na shughuli zao za kawaida, bila kujali kuhusu matokeo yanayoendelea kutolewa na IEBC katika ukumbi wa Bomas, Nairobi.

Wale waliozungumza na ‘Taifa Jumapili’ walisema kuwa licha ya ahadi nyingi wanazopewa na wanasiasa, ni jukumu lao kujitafutia riziki ya kila siku.

“Tunachoomba ni uwepo wa amani. Tunawarai viongozi wanaoshindwa kukubali matokeo ya uchaguzi au kwenda mahakamani kuwasilisha malalamishi yao badala ya kuwatumia vijana kuvuruga amani. Kwa sasa kila mtu anahangaika kuhusu vile atailisha familia yake kutokana na gharama ya juu ya maisha,” akasema Bi Mary Nkatha, ambaye ni mchuuzi katika mtaa mmoja jijini Nairobi.

Wakenya wengi walisema kuwa kila mmoja anapaswa kujifunza na matukio yaliyoshuhudiwa nchini, hasa kwenye chaguzi kuu za 2017 na 2007, ambapo mamia ya watu walipoteza maisha yao kutokana na ghasia za kisiasa na kikabila.

Hapo jana, viongozi wa kidini waliwarai Wakenya kuendelea kuzingatia amani, kwani maisha yao yataendelea kama kawaida bila kujali yule atakayetangazwa kuwa rais mpya.

“Amani ndiyo nguzo pekee tutakayojivunia kama nchi,” akasema Askofu Mstaafu David Oginde, kwenye taarifa aliyosoma kwa niaba ya viongozi hao.

  • Tags

You can share this post!

Mvurya awazidi maarifa Joho na Kingi, Achani akichukua Kwale

Ndiritu Muriithi aisuta IEBC kwa kuwafungia nje ya Bomas

T L