Nani safi kati ya Raila na Ruto?

Nani safi kati ya Raila na Ruto?

Na BENSON MATHEKA

NAIBU Rais William Ruto na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga wamelaumiana kwa ufisadi, kila mmoja akitaka kumpaka tope mwenzake uchaguzi mkuu wa 2022 ukikaribia.

Mwishoni mwa wiki, viongozi hao walielekezeana madai ya ufisadi Bw Odinga aliposema kwamba akiingia mamlakani, serikali yake itawafunga jela viongozi wote wafisadi.

Ingawa wawili hao wamekuwa wakilaumiana, wote wawili wamehusishwa na sakata za ufisadi na baadhi ya wandani wanaowazunguka wameshtakiwa kwa madai ya ufisadi.

Dkt Ruto, ambaye amehusishwa na kashfa za ardhi ikiwemo ya unyakuzi wa shamba la mkimbizi wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007, Adrian Muteshi anazungukwa na washirika wanaohusishwa na madai ya ufisadi.

Mbali na kesi ya shamba la Muteshi alilorudisha baada ya kupatikana na hatia kortini, Dkt Ruto amehusishwa na madai ya unyakuzi wa shamba la shule ya msingi ya Langata, Nairobi kupitia hoteli yake ya Weston, unyakuzi wa ardhi ya kampuni ya mabomba ya mafuta ya Kenya na ya Mamlaka ya Viwanja vya ndege ambayo hoteli ya Weston imejengwa.

Alilaumiwa kwa kutetea sakata ya mabwawa ya Kimwarer na Arror ambapo serikali ya Kenya ilipoteza zaidi ya Sh20 bilioni kulingana na ripoti ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma.

Aliyekuwa waziri wa Fedha Henry Rotich ameshtakiwa kwa madai ya kuhusika katika kashfa hiyo.

Washirika wake ambao wanakabiliwa na kesi za ufisadi ni pamoja na mbunge wa Malindi Aisha Jumwa, mbunge wa Sirisia John Walukhe na mbunge wa Kimilili Didmus Barasa.

Wengine ni mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya anayekabiliwa na kesi ya ulaghai na Mbunge wa Mathira Rigathi Gachagua anayechunguzwa kwa madai ya ufisadi anayodai ni ya kisiasa.

Bw Odinga naye amekuwa akihusishwa na madai ya kupotea kwa pesa za mpango wa Kazi kwa Vijana uliokuwa chini ya ofisi ya waziri mkuu katika serikali aliyogawana mamlaka na rais mstaafu Mwai Kibaki.

Familia yake imekuwa ikitajwa katika kashfa ya ununuzi wa kiwanda cha Kisumu Mollases mjini Kisumu, madai ambayo pia hayajawahi kuthibitisha au familia yake kushtakiwa.

Familia ya Bw Odinga imekanusha kwamba ilitumia njia za mkato kununua kiwanda hicho.Kabla ya uchaguzi mkuu wa 2017, kampuni ya mashamba ya Dominion inayohudumu eneo la Nyanza, ilidai kwamba Bw Odinga alimuitisha hongo ya Sh200 milioni ili isitimuliwe kutoka shamba noja la mchele.

Afisa mkuu wa kampuni hiyo Calvin Burgess alidai kwamba shida ilianza alipokataa kufadhili chama cha ODM.Mnamo 2011, familia ya Bw Odinga ilitajwa kwenye sakata ya mahindi ya Sh2 bilioni wakati ambao Dkt Ruto alikuwa waziri wa Kilimo.

Kwenye nyaraka za siri ambazo zilifichuliwa na Wikileaks, aliyekuwa balozi wa Amerika nchini Michael Ranneberger aliambia serikali yake kwamba Raila alitaka kumpaka tope Dkt Ruto ilhali ni familia yake iliyohusika na sakata hiyo.

Washirika wa karibu wa Bw Odinga akiwemo aliyekuwa gavana wa Nairobi Evans Kidero na gavana wa Busia Sospeter Ojaamong wanakabiliwa na kesi za ufisadi mahakamani.

Ingawa amekuwa akikemea wandani wa Dkt Ruto wanaoshtakiwa, hajawahi kuwakemea magavana hao, na kujitenga nao.

Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino ambaye ni mmoja wa watetezi wakuu wa Bw Odinga pia anakabiliwa na kesi ya kujaribu kuua.

You can share this post!

MARY WANGARI: Utafiti mpya wahimiza manufaa ya kupokea...

Tanzania mbioni kuunda chanjo yake ya corona