Habari MsetoSiasa

Naogopa Mungu na uji moto pekee, Waititu aropokwa

May 27th, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

GAVANA wa Kiambu Ferdinand Waititu sasa anasema kuwa hakuna mtu atakayemlazimisha kukoma kumuunga mkono Naibu Rais William Ruto ili ampigie debe kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga, akisema hamwogopi yeyote.

Akidai kuwa mavamizi maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) nyumbani kwake majuzi, gavana huyo alidai kuwa matukio hayo yalikuwa yakimtendekea kutokana na hali yake ya kumuunga Dkt Ruto mkono lakini akasema hataacha.

Alisema “hata haya mambo mnasikia kuwa wasichana wangu wana mamilioni katika akaunti na kuwa nina akaunti 50, ni hawa watu wananipiga kwa kuwa niko Tangatanga.”

Lakini aliapa kuwa yeye si mwoga, akisema, “Mimi siwezi kufuata Raila kwa nguvu, hakuna mtu anaweza kunilazimisha. Kwa sababu mimi naogopa Mungu na uji moto peke yake.”

Gavana huyo alieleza hadhira jinsi Mungu amemtoa mbali, na kuwa hataruhusu aangushwe wakati huu.

“Na mimi unajua ni mtu ambaye Mungu amemsaidia sana katika dunia hii. Amenitoa katika mitaa ya mabanda, sasa nimeenda hivi hadi nikawa gavana. Na hata hawa wananikujia sahii, mimi najua Mungu ataniondolea,” akasema Bw Waititu, ambaye anachunguzwa kuhusiana na madai ya ufisadi.