Michezo

Naomi Osaka ana hela za kukausha bahari licha ya umri mdogo

September 9th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

NAOMI Osaka, 22, ni mwanatenisi maarufu raia wa Japan aliyewahi kuorodheshwa nambari moja duniani na Shirikisho la Tenisi ya Wanawake Duniani (WTA).

Ndiye mwanatenisi wa kwanza mzawa wa bara Asia kuwahi kushikilia nafasi ya kwanza duniani katika tenisi ya mchezaji mmoja kila upande.

Kufikia sasa, anajivunia kutia kibindoni mataji matano ya WTA Tour. Alijinyakulia mataji mawili ya kwanza ya Grand Slam kwa mchezaji mmoja kila upande kwa kutawala vipute vya US Open na Australian Open mnamo 2018 na 2019 mtawalia. Ndiye mchezaji wa kwanza baada ya Jennifer Capriati mnamo 2001 kufikia mafanikio hayo.

Baba wa Osaka ana usuli nchini Haiti na mamake ni mzawa wa Japan. Hata hivyo, Osaka aliishi na kukulia nchini Amerika alikopokezwa malezi ya tenisi tangu akiwa na umri wa miaka mitatu.

Umaarufu ulianza kumwandama akiwa na umri wa miaka 16 alipombwaga aliyekuwa bingwa mtetezi wa WTA Tour, Samantha Jane Stour wa Australia katika kivumbi cha Stanford Classic mnamo 2014.

Miaka miwili baadaye, alitinga fainali ya WTA kwa mara ya kwanza na kutamalaki kipute cha Pan Pacific Open 2016. Ushindi huo ulimweka ndani ya orodha ya wanatenisi 50-bora kwenye msimamo wa WTA.

Alitikisa dunia mnamo 2018 kwa kumlaza bingwa mara 23 wa Grand Slam, Serena Williams, 38, katika fainali ya US Open. Ufanisi huo ulimfanya Mjapani wa kwanza kuwahi kuibuka mshindi wa Grand Slam kwa mchezaji mmoja kila upande.

Osaka anafahamika zaidi kwa ukali wa mipakuo yake na fataki yake moja ina uwezo wa kufikia umbali wa kilomita 200 kwa kipindi cha dakika 60.

UTAJIRI

Osaka kwa sasa ndiye mwanamichezo wa kike anayevutia zaidi kibiashara duniani. Isitoshe, ndiye mwanamichezo wa kike anayelipwa mshahara mnono zaidi duniani. Anashikilia nafasi ya 29 kati ya wanaspoti wanaodumishwa kwa ujira mkubwa zaidi kimataifa.

Mnamo Mei 2020, Jarida la Forbes lilifichua kwamba Osaka alikomesha ukiritimba wa miaka minne wa Serena wa kuwa mwanamichezo wa kike anayelipwa vyema zaidi duniani baada kujizolea jumla ya Sh4.3 bilioni. Fedha hizo zilizidi zile alizopata Serena mnamo 2019 kwa takriban Sh161 milioni.

Osaka amekuwa balozi wa mauzo wa kampuni ya vifaa ya masuala ya usimamizi nchini Japan, IMG, tangu 2016.

Kampuni ya vifaa vya michezo ya Yonex nchini Japan imekuwa ikimpokeza Osaka raketi za tenisi tangu 2008.

Hadi kufikia sasa, yeye hutumia raketi aina ya Yonex Ezone 98. Nyuzi za raketi hiyo ni za aina ya Polytour Pro 125 na Rexis 130.

Osaka amekuwa pia balozi wa mauzo wa kampuni nyingine ya vifaa vya michezo ya Nike tangu 2019.

Hadi alipotia saini mkataba wa miaka mitano na Nike, alikuwa balozi wa mauzo wa kampuni ya Adidas iliyokuwa ikimpokeza kima cha Sh30 milioni kwa mwezi kwa kipindi cha miaka minne.

Osaka pia hujirinia fedha za ziada kwa kuwa balozi wa mauzo wa kampuni ya magari ya Nissan na kampuni ya vifaa vya kielektroniki ya Citizen Watch.

Yeye pia ni balozi wa mauzo wa kampuni za vyakula ya Nissin Foods, kampuni ya vipodozi ya Shiseido, shirika la utangazaji la Wowow na kampuni ya safari za ndege ya Nippon Airways (ANA).