Michezo

Napenda mbinu za Sarri, asema Hazard licha ya kumumunywa 6-0 na Man City

February 14th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

LICHA ya Chelsea kumumunywa na Man City kama pipi mabao sita bila jibu, winga matata wa Chelsea Eden Hazard amesifu utendakazi wa kocha Maurizio Sarri huku madai yakiendelea kushika kasi kwamba Mtaliano huyo huenda akatimuliwa kutokana na matokeo mabaya ya Chelsea katika mechi zilizopita.

Hazard amesema kwamba mtindo wa soka wanaofundishwa na Sarri ndio bora zaidi tangu atue Uingereza kusakatia Chelsea na kwenye taaluma yake nzima ya soka.

“Makocha wote walionifunza soka wamenipa kitu cha kujivunia. Tangu enzi za Claude Puel nikiwa Lille hadi sasa Maurizio Sarri, nimegundua kwamba makocha huwa na mbinu na mtazamo tofauti wa soka,” akatanguliza.

“Jose Mourinho alikuwa kocha wa kipekee lakini jinsi makocha Sarri na Rudi Garcia (mkufunzi wa zamani wa Lille) wanavyoelekeza wachezaji kuwajibika uwanjani inapendeza sana na nakumbatia mbinu zao kuliko kocha yeyote niliyowahi kupitia mikononi mwake,” akaendeleza Hazard.

Ripoti za kuondoka kwa Sarri pia zimekuwa zikimwandama Hazard ambaye amekuwa akidaiwa analenga kuhamia kambini mabingwa watetezi wa Kombe la Klabu Bingwa Barani Uropa Real Madrid ya Uhispania.

Uhamisho umekuwa ukidaiwa utagharimu kiasi kubwa cha fedha na hata kutajwa kama utakaokuwa ghali zaidi duniani kwenye fani ya soka.

Kichapo cha Man City kilikuwa cha nne kwa Chelsea katika mechi nne za ligi za hivi punde walizokuwa wamesakata.

Sarri alianza msimu wa 2018/19 wa EPL kwa kishindo baada ya kuwaongoza Chelsea kuandikisha rekodi ya kutoshindwa kwa mechi 12 za kwanza lakini mambo sasa yamemgeuka na mashabiki wa timu hiyo kuanza kumchoka.