Michezo

Napoli wabadilisha jina la uwanja wao wa San Paolo hadi Diego Armando Maradona Stadium

December 5th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

NAPOLI wamebadilisha jina la uwanja wao wa nyumbani wa Stadio San Paolo na kuuita Diego Maradona kwa heshima ya jagina huyo wa soka.

Maradona ambaye ni mshambuliaji na kocha wa zamani wa Argentina aliaga dunia mnamo Novemba akiwa na umri wa miaka 60. Katika enzi yake ya usogora, aliongoza Napoli kutwaa mataji mawili ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mnamo 1987 na 1990.

Hatua ya uwanja wa San Paolo kubadilishwa jina hadi Diego Armando Maradona tayari imeidhinishwa na manispaa ya jiji la Naples.

Pendekezo la kubadilishwa kwa jina la uwanja huo lilitolewa na rais wa Napoli, Aurelio de Laurentiis wakati akimwomboleza Maradona aliyeaga dunia kutokana na maradhi ya moyo yaliyochangiwa na uraibu wa kutegemea zaidi matumizi ya dawa za kulevya.

Pendekezo la De Laurentiis liliungwa mkono na Meya wa zamani wa jiji la Naples, Luigi de Magistris.

Maradona alihudumu kambini mwa Napoli kwa kipindi cha miaka saba baada ya kubanduka kambini mwa Barcelona mnamo 1984. Akivalia jezi za miamba hao wa soka ya Italia, pia aliwaongoza kutwaa taji la Coppa Italia mnamo 1987 na taji la Uefa Cup mnamo 1989.

Idadi kubwa ya mashabiki walijitokeza katika uwanja wa San Paolo baada ya kufa kwa Maradona mnamo Novemba 25, 2020 huku kikosi cha Napoli kikichukua muda kumwomboleza kabla ya mechi ya Europa League iliyowakutanisha na HNK Rijeka ya Croatia mnamo Novemba 26, 2020 ugani Sao Paolo. Kila mchezaji wa Napoli alivalia jezi yenye maandishi ‘Maradona 10’ mgongoni.

“Maradona ndiye mchezaji bora wa muda wote duniani. Alijivunia kipaji na talanta adimu na kipaji adhimu kilichompa ushawiki mkubwa kambini mwa Napoli kwa miaka saba. Alikuwa kipenzi kikubwa cha mashabiki wa soka jijini Naples,” ikasema sehemu ya taarifa ya kikosi cha Napoli.

Maradona alichezea Napoli mara 188 na kufunga mabao 81. Idadi ya mechi alizosakatia Napoli ndiyo kubwa zaidi kwa nguli huyo kuwahi kuchezea kikosi chochote kingine kilichowahi kujivunia maarifa yake.

Maradona aliwahi pia kuvalia jezi za Argentina katika fainali nne za Kombe la Dunia na alikuwa nahodha wa timu hiyo walipotwaa ubingwa mnamo 1986 nchini Mexico.