Napoli walima Lazio 5-2 huku Atalanta wakitoshana nguvu na AS Roma kwenye Serie A

Napoli walima Lazio 5-2 huku Atalanta wakitoshana nguvu na AS Roma kwenye Serie A

Na MASHIRIKA

NAPOLI waliwapepeta Lazio 5-2 katika mechi ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mnamo Alhamisi usiku na kupunguza pengo la alama kati yao na viongozi wa jedwali Inter Milan hadi pointi 13.

Penalti kutoka kwa Lorenzo Insigne na goli jingine kutoka kwa fowadi Matteo Politano liliwezesha Napoli kujiweka uongozini mapema kabla ya Insigne kupachika wavuni goli la tatu la waajiri wake.

Mabao mengine ya Napoli yalijazwa kimiani na Dries Mertens na Victor Osimhen ambaye ni raia wa Nigeria. Goli la Mertens ambaye ni raia wa Ubelgiji, lilimfanya kufikia rekodi ya Antonio Vojak ambaye kwa pamoja naye, sasa ni wafungaji bora wa muda wote (mabao 102 katika Serie A) kambini mwa Napoli.

Lazio walijibu mapigo ya Napoli kupitia wanasoka Ciro Immobile na Sergej Milinkovic-Savic waliofunga mabao mawili chini ya dakika tatu za kipindi cha pili.

Kufikia sasa, Napoli wanashikilia nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali la Serie A kwa alama 63, mbili nyuma ya mabingwa watetezi Juventus na Atalanta walioambulia sare ya 1-1 dhidi ya AS Roma.

Lazio kwa upande wao wanakamata nafasi ya sita kwa alama 58 japo wana mchuano mmoja zaidi wa kusakata ili kufikia idadi ya mechi 32 ambazo zimepigwa na klabu tano za kwanza jedwalini, ikiwemo nambari mbili AC Milan.

Ushindi wa Napoli ulitamatisha rekodi nzuri ya Lazio ambao walishuka dimbani wakijivunia ufanisi wa kushinda jumla ya mechi tano mfululizo. Sasa wana fursa ya kupaa zaidi jedwalini iwapo watawakomoa AC Milan wanaojivunia pointi 66 watakapokutana jijini Roma mnamo Aprili 26, 2021.

Wakicheza dhidi ya Roma ugenini, Atalanta walikamilisha mchuano na wanasoka 10 pekee uwanjani baada ya kiungo Robin Gosens kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 69.

Ruslan Malinovskiy aliwaweka Atalanta kifua mbele kabla ya Roma ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya saba kwa alama 55 kusawazishiwa na Bryan Cristante kunako dakika ya 75.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kipa Matasi amezewa mate na miamba wa TZ na Zambia

MKU yashirikiana na KFS kutekeleza miradi ya upanzi wa miti