Napoli watandika AS Roma na kufungua pengo la alama 13 kileleni mwa jedwali la Serie A

Napoli watandika AS Roma na kufungua pengo la alama 13 kileleni mwa jedwali la Serie A

Na MASHIRIKA

BAO la dakika za mwisho kutoka kwa Giovanni Simeone liliwezesha Napoli kucharaza AS Roma 2-1 katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A) na kufungua pengo la alama 13 kati yao na nambari mbili Inter Milan kileleni mwa jedwali.

Victor Osimhen aliwaweka Napoli uongozini mwanzoni mwa kipindi cha kwanza kabla ya Roma ya kocha Jose Mourinho kusawazishiwa na Stephan El Shaarawy.

Napoli wanaofukuzia taji la Serie A kwa mara ya kwanza tangu 1990, sasa wanadhibiti kilele cha jedwali la Serie A kwa alama 53 baada ya mechi 20. Roma wanashikilia nafasi ya sita kwa pointi 37, moja pekee nyuma ya Lazio, Atalanta na mabingwa watetezi AC Milan waliokubali kichapo cha 5-2 kutoka kwa Sassuolo ugani San Siro.

Huku Lazio wakiambulia sare ya 1-1 dhidi ya Fiorentina, Juventus walishuka hadi nafasi ya 13 kwa pointi 23 baada ya Monza kuwapiga 2-0 jijini Turin.

Ilikuwa mara ya kwanza tangu Aprili 1997 kwa Milan kufungwa mabao matano katika pambano moja la Serie A nyumbani. Chini ya kocha Stefano Pioli, miamba hao hawajashinda mechi yoyote kati ya nne zilizopita ligini A na wameokota mpira kimiani mara 12 kutokana na mechi tatu zilizopita katika mashindano yote.

“Lazima tuzinduke japo huenda tusifaulu kutawazwa wafalme wa Serie A muhula huu. Hata hivyo, lazima tupiganie fursa ya kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao,” akasema Pioli.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

  • Tags

You can share this post!

Kenya Kwanza yataka kampuni za Uhuru zianze kulipa ushuru

TAHARIRI: Changamoto za CBC zilizobaki zitatuliwe

T L