Napoli yatoka nyuma na kudhalilisha Ajax mbele ya mashabiki wao wa nyumbani katika UEFA

Napoli yatoka nyuma na kudhalilisha Ajax mbele ya mashabiki wao wa nyumbani katika UEFA

Na MASHIRIKA

NAPOLI walitoka nyuma na kudhalilisha Ajax kwa kichapo cha 6-1 katika pambano la Kundi A kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Jumanne usiku jijini Amsterdam.

Mohammed Kudus aliwaweka Ajax kifua mbele katika dakika ya tisa kabla ya Giacomo Raspadori kusawazisha mambo kunako dakika ya 18. Giovanni di Lorenzo alifunga goli la pili la Napoli katika dakika ya 33 kabla ya Piotr Zielinski kufanya mambo kuwa 3-1 mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Raspadori alifunga bao la nne la Napoli kabla ya kuandalia Khvicha Kvaratskhelia krosi safi iliyozalisha goli la tano.

Dusan Tadic wa Ajax alionyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 73 kabla ya Giovanni Simeone kuwafungia Napoli goli lao la sita.

Napoli, waliotumia chipukizi wengi kujaza nafasi ya vigogo mwanzoni mwa msimu huu, hawajapoteza mchuano wowote katika mapambano yote ya muhula huu.

Chini ya kocha Luciano Spalletti, kikosi hicho kinaselelea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) na Kundi A la UEFA kwa mabao 13 kutokana na mechi tatu. Sasa wana alama tisa, tatu zaidi kuliko Liverpool waliokomoa Rangers ya Scotland 2-0 katika mchuano mwingine wa Kundi A mnamo Jumanne usiku ugani Anfield.

Kichapo kutoka kwa Napoli ndicho kinono zaidi kwa Ajax kuwahi kupokezwa katika soka ya bara Ulaya. Aidha, ndicho kichapo kinono zaidi katika historia yao kwenye mashindano yoyote tangu 1964. Ni kichapo cha pili kinono zaidi kwao katika mechi ya nyumbani.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Wakulima wa pamba iliyoimarishwa walia kukawia kwa mbegu

Tottenham na Frankfurt waumiza nyasi bure katika pambano la...

T L